Abjadi
Abjad ni jina la mwandiko wa lugha ya Kiarabu na pia jina la kundi la miandiko inayotumia muundo wa kuandika konsonanti za neno lakini kuacha vokali.
Jina la mwandiko wa Kiarabu
Neno "abjad" linajumuisha herufi 4 za kwanza ابجد a-b-j-d za mwandiko wa Kiarabu sawa kama "a-b-c" inamaanisha herufi 3 za kwanza za alfabeti ya Kilatini.
Abjadi ilikuwa pia jina la muundo wa namba za Kiarabu kabla ya kupokewa kwa namba za Kihindi wakati wa karne ya 9 BK/ 3 BH; hadi wakati ule Waarabu walitumia alama za mwandiko kwa ajili ya mahesabu.
Jina la kundi la miandiko ya lugha za Kisemiti
Mbali na kutaja mwandiko wa Kiarabu neno hili latumiwa pia kwa kutaja tabia za miandiko ya lugha mbalimbali za Kisemiti. Zote zina alama kwa ajili ya konsonanti lakini kwa kawaida vokali haziandikwi.
Hapa msomaji anatakiwa kutambua neno na kujua ni vokali zipi zinazosomwa pamoja na konsonanti zilizoandikwa.
Lugha hai zinazotumia muundo wa abjadi ni Kiarabu, Kiebrania na Kiaramu ambazo zote ni lugha za Kisemiti. Lugha nyingi za Kisemiti za kihistoria zisizo na wasemaji tena zilituma pia mwandiko wa abjadi.
Mwandiko wa abjadi wa kwanza ilikuwa herufi za Kifinisia.
Abjadi za kisasa huwa na uwezekano kuandika vokali pia lakini zinachapishwa tu katika vitabu vya watoto wadogo wanaoanza kusoma au kwa maneno machache yenye matamshi tofauti lakini konsonanti sawa.
Abjadi kama muundo wa mwandiko kwa lugha zisizo Kisemiti
Kusoma mwandiko wa abjadi kunaleta matatizo zaidi kuliko kusoma alfabeti au abugida kwa sababu herufi zinaonyesha sehemu ya matamshi tu.
Kutokana na uenezaji wa Uislamu uliotumia Kiarabu kama lugha ya kimataifa kuna pia lugha nyingine zisio Kisemiti zinazoandikwa kwa kutumia herufi za Kiarabu na hizi ni hasa Kiajemi, Kidari, Kikurdi, Kiurdu, Kipanjabi, Kisindhi na Kipashto yaani lugha katika eneo kati ya Irak hadi Uhindi.
Tangu karne ya 20 lugha nyingi ambazo si za Kisemiti zimeacha kutumia abjadi yaani herufi za Kiarabu: kwa mfano Kiswahili na Kituruki zikahamia matumizi ya alfabeti ya Kilatini.
Tazama pia
Vitabu
- Peter T. Daniels, William Bright: The Worlds Writing Systems; New York: Oxford University Press, 1995; ISBN 0-19-507993-0
- Н. В. Юшманов: Грамматика Литературного Арабского Языка (N. V. Yushmanov: Grammatika Literaturnogo Arabskogo Yazyka; Moskau: Verlag „Nauka“, 1985; S. 30