Fasihi simulizi

mighani

Fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia mdomo (tofauti na maandishi kama kwenye fasihi andishi) kama njia kuu ya kufikisha ujumbe. Ni sehemu ya msingi ya utamaduni na vipengele vyake vingi vinafanya kazi kama katika fasihi kwa jumla.

Katika jamii isiyo na uandishi ni wazi kuwa hakuna fasihi andishi. Hata hivyo kila jamii ina hazina ya mapokeo yapokelewayo Kwa mdomo na kihifadhiwa katika maandishi kwa mfano: utenzi, ngano au nyimbo za jadi. Hivyo vyote ni sehemu za fasihi simulizi.

Hata jamii ijuayo kusoma na kuandika inaendelea kuwa na fasihi simulizi, hasa nyumbani, k.m. katika kuwasimulia watoto hadithi. Lakini mara nyingi fasihi simulizi ya jamii ijuayo kusoma na kuandika ni tofauti sana na fasihi simulizi ya jamii isiyo na uandishi, kwa vile imeathiriwa na ujuzi wa kusoma na kuandika, na mitindo ya masimulizi yake hayaendi sambamba na mitindo ya masimulizi yasiyoathiriwa na uandishi.

Sifa za fasihi simulizi

Fasihi simulizi ina sifa za kipekee ambazo huipambanua na fasihi andishi. Sifa hizo ndizo huipa uhai fasihi hii. Miongoni mwa sifa hizo ni pamoja na:

  1. Utendaji wa fasihi simulizi hushirikisha utendaji wa fanani na hadhira moja kwa moja (ana-kwa-ana)
  2. Fanani kuwepo kwa fanani ambaye husimulia, huimba, hupiga makofi na kubadilisha miondoko na mitindo ya usimuliaji.
  3. Hadhira kuwepo kwa hadhira ambayo hushiriki kwa kuuliza maswali, kupiga makofi, kushangilia, kuimba, kuiga na kadhalika - kutegemea jinsi ambavyo fanani atawashirikisha.
  4. Fasihi simulizi huingiliana na mabadiliko ya kiwakati na kimazingira; baadhi ya tanzu au vipera vya fasihi simulizi vinaweza kuwa vimepitwa na wakati lakini bado vinaweza kubadilishwa na vikaafikiana na wakati mahususi.
  5. Fasihi simulizi ni mali ya jamii nzima, humilikiwa na kila mtu katika jamii. Sifa hii ndiyo huipa uwezo wa kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
  6. Fasihi simulizi huzaliwa, hukua na hata hufa. Kuzaliwa: fasihi simulizi huzaliwa kutokana na mambo yanayotokea katika jamii. Kukua: fasihi simulizi hukua kadri inavyojadili matatizo yanayojitokeza. Kufa: fasihi simulizi hufa kwa namna mbili. Hii ni kutokana na maendeleo ya mazingira ambayo hufuata mfumo wa jamii husika. Kwa mfano kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia fasihi inaweza kuhifadhiwa kwenye maandishi na kwenye kanda mbalimbali za kurekodi.
  7. Fasihi simulizi ina mandhari maalumu ya kutendea; ni sehemu ambayo imetengwa rasmi kwa ajili ya aina/kipera fulani cha fasihi simulizi. Mandhari hayo yanaweza kuwa porini, misituni, mtoni, pangoni, nyumbani na kadhalika.
  8. Fasihi simulizi ina sifa ya "kuwa na utegemezi".Utegemezi wa fasihi simulizi hutegemea zaidi sanaa za maonesho hasa sanaa za ghibu yaani muziki,kwa sababu,fasihi simulizi huchota uhai wake kutokana na vitendo na tabia za fanani,mahadhi na toni za kimuziki na vipengele vingine vya sanaa za maonesho.

Tanzu na vipera vya fasihi simulizi

HadithiUshairiSemisanaa za maonesho
NganoMashairiMethaliMatambiko
ViganoTenziNahauMajigambo
SogaTendiMisemoMivigha
VisakaleNgonjeraMafumboUtani
VisasiliNyimboVitendawiliVichekesho
HekayaMaghaniMizunguNgoma
HurafaMichezo ya jukwaani
Michezo ya watoto
Ngonjera
Maigizo

Hadithi

Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake huwa mwepesi au sahili. Urefu wa hadithi hutofautiana kutoka kitanzu/kipera kimoja hadi kingine. Kwa jumla zipo hadithi ambazo ni za kubuni na zingine za kihistoria.

Baadhi ya vipera vya utanzu huu ni:

Ngano

Hizi ni hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama, miti na watu katika kuelezea au kuonya kuhusu maisha. Vijipera vya kipera hiki ni:

Soga

Ni hadithi ndogo ndogo zinazohusisha utani na ucheshi kwa kiasi fulani. Hizi ni hadithi ambazo hutambwa katika mtiririko wa matukio ambao huzua kicheko. Soga hudhamiria kuchekesha na pia kukejeli.

Visakale

Masimulizi ya kimapokeo juu ya wahenga au mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia. Kwa mfano hadithi za Liyongo.

Mapisi

Maelezo ya historia bila kutia mambo ya kubuni.

Tarihi

Hizi ni hadithi ambazo husimulia au zimejengwa kwenye matukio ya kihistoria. Inawezekana matukio yanayosimuliwa yakawa ya kweli, yaani yalipata kutokea kihistoria. Hadithi hizi hutokea zaidi katika maandishi.

Visasili

Ni utanzu unaofungamana na imani za dini na mizungu ya jamii. Hizi ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii inayohusika kuhusu asili ya ulimwengu na mwenendo wake, kuhusu asili yao wenyewe, na maana na shabaha ya maisha yao. Mara nyingi hadithi hizi huaminiwa kuwa ni kweli tupu, na hutumika kuelezea au kuhalalisha baadhi ya mila na madhehebu ya jamii inayohusika.

Ushairi

Huu ni utanzu wa fasihi simulizi unaowasilishwa kwa hadhira kwa njia ya uimbaji au ughani badala ya usemaji wa kawaida. Katika utanzu huu kuna vipera viwili ambavyo ni nyimbo na maghani.

Nyimbo

Nyimbo ni kila kinachoimbwa. Kipera hiki kimegawanyika katika vijipera vifuatavyo ambavyo ni, tumbuizo, bembea, kongozi, nyimbo za dini, wawe, tenzi, tendi, mbolezi, kimai, nyiso, nyimbo za vita, nyimbo za uwindaji, nyimbo za taifa.

Maghani

Maghani ni istilahi inayotumiwa kuelezea aina ya ushairi ambao hutolewa kwa kalima au maneno badala ya kuimbwa. Kipera hiki kina vijipera vitatu ambavyo ni maghani ya kawaida, sifo na maghani masimulizi.

Maghani ya kawaida

Hilo ni kundi ambalo tunaweza kuingiza fani mbalimbali za ushahiri simulizi kama vile ushairi wa mapenzi, siasa, maombolezo, kazi, dini ilimradi unaghanwa katika namna ya uwasilishwaji wake.

Sifo

Hizi ni tungo za kusifu ambazo husifu watu, wanyama na mimea. Baadhi ya sifo huwa zinakashifu au kukejeli. Sifo huwa na tanzu muhimu kama vile vivugo (majigambo), pembezi na tondozi.

Semi

Semi ni tungo au kauli fupifupi za kisanaa zitumiazo picha na tamathali kuelezea maudhui yanayobeba maana au mafunzo muhimu kwa jamii. Kundi hili lina vipera au tanzu sita ambazo ni:

  • Methali
  • Vitendawili
  • Nahau
  • Misemo
  • Mafumbo
  • Mizungu
  • Lakabu

Methali

Methali ni semi fupi fupi zenye mpangilio maalumu wa maneno ambazo huelezea kwa muhtasari mafunzo, mafumbo na mawazo mazito yaliyotokana na uzoefu wa kijamii. Mara nyingi mawazo hayo huelezwa kwa kutumia tamathali hasa sitiari na mafumbo.

Methali nyingi huundwa na vipande viwili vya maneno vyenye fikra yurani. Kipande cha kwanza huashiria tendo au sharti na kipande cha pili huashiria matokeo ya tendo au sharti hilo. Au sehemu ya kwanza huanzisha wazo fulani, na sehemu ya pili hulikanusha au kulikamilisha wazo hilo. Kwa mfano; mwenda pole hajikwai, aliye juu mngoje chini.

Mifano ya methali
  • Mcheka kilema,hali hakija mfika.
  • Kupotea njia, ndiko kujua njia.
  • Mchelea mwana kulia, utalia wewe.

Maana ya methali hutegemea muktadha au wakati maalumu katika jamii.

Kazi za methali

Methali zina kazi nyingi katika jamii yoyote ile kama vile:

  • Kuionya jamii inayohusika au inayopewa methali hiyo.
  • Kuishauri jamii inayopewa au kutamkiwa methali hiyo.
  • Kuihiza jamii inayohusika.
  • Kukejeli mambo mbalimbali yanayofanyika ndani ya jamii husika.

Vitendawili

Ni semi zilizofumbwa ambazo hutolewa kwa hadhira ili izifumbue. Fumbo hilo kwa kawaida huwa linafahamika katika jamii hiyo, na mara nyingi lina mafunzo muhimu kwa washiriki, mbali na kuwachemsha bongo zao. Vitendawili ni sanaa inayotegemea uwezo wa mtu kutambua, kuhusisha na kulinganisha vitu vya aina mbalimbali vilivyomo katika maumbile.

Misimu

Ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. Msimu ukipata mashiko ya kutosha katika jamii huweza hatimaye kuingia katika kundi la methali za jamii hiyo.

Mafumbo

Ni semi za maonyo au mawaidha ambazo maana zake za ndani zimefichika. Fumbo hubuniwa na msemaji kwa shabaha na hadhira maalum, hivyo ni tofauti na methali au vitendawili ambavyo ni semi za kimapokeo.

Lakabu

Haya ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Majina haya huwa ni maneno au mafungu ya maneno yenye maana iliyofumbwa. Mara nyingi majina haya huwa ni sitiari. Baadhi ya majina haya humsifia mhusika, lakini mengine humkosoa au hata kumdhalilisha; Mifano: simba wa yuda- Hali Selassie, Baba wa taifa – Mwl Nyerere.

Sanaa za maonyesho.

Ni maonesho au maigizo ambayo hutumia watendaji na mazingira maalumu kwa kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani kwa hadhira.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Fasihi simulizi kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.