Kaunti za Kenya

maeneo ya Kwanza ya kiutawala

Kaunti za Kenya (en: Counties of Kenya) ni maeneo ya kiutawala ya Kenya tangu kuadhimishwa kwa katiba ya mwaka 2010[1].

Kaunti za Kenya.

Katiba hiyo inaeleza kuwepo kwa kaunti 47 nchini katika mafungu 191 na 192, pamoja na ‘County Governments Act of 2012”. Kaunti hizi zilichukua nafasi za Mikoa ya Kenya. Mipaka ya kaunti iliwekwa kulingana na mipaka ya wilaya za kenya zilizokuwa zimeanzishwa kisheria mwaka wa 1992.

Mipaka ya kaunti hizo ni pia msingi wa maeneo ya uchaguzi wa mwakilishi mwanamke wa kaunti, seneta na gavana. [2][3]

Serikali

Utendaji katika Kaunti

Utendaji wa kaunti una wajibu wa kutekeleza madaraka ya serikali ya kaunti. Gavana ndiye mtendaji mkuu na husaidiwa na naibu wa gavana. Kila kaunti ina kamati ya utendaji iliyoundwa na[4]:

  • Gavana
  • Naibu wa gavana
  • Kamati ya watu wasiozidi thuluthi ya wabunge wa kaunti au watu kumi, ambapo bunge la kaunti lina watu zaidi ya 30
  • Katibu wa kaunti

Kazi ya utendaji ni:

  • Kutekeleza sheria za bunge la kaunti
  • Kutekeleza sheria za kitaifa ndani ya mipaka ya kaunti
  • Kuendesha na kuratibu shughuli za utawala wa kaunti na idara zake
  • Kutayarisha miswada ya sheria na kuzipeleka katika bunge la kaunti
  • Kuwajibika kwa bunge la kaunti na wananchi wa kaunti

Bunge la Kaunti

Kila kaunti ina bunge. Wajumbe huchaguliwa kutoka wadi za kaunti katika uchaguzi mkuu. Pia, kuna wajumbe wa kuteuliwa ambao huwakilisha vikundi vilivyotengwa, vijana na kwa ajili ya kusawazisha uwakilishi wa jinsia. Wajumbe hutumikia kwa muhula wa miaka mitano. Bunge huongozwa na spika ambaye hafai kuwa mjumbe.

Majukumu yake ni:

  • kuchuja na kuthibitisha waliopendekezwa kuteuliwa katika ofisi za umma katika kaunti
  • Kutengeneza sheria za kaunti
  • kuthibitisha bajeti na matumizi ya serikali ya kaunti
  • kuthibitisha mikopo ya kaunti
  • kuthibitisha mipango ya maendeleo ya kaunti
  • kuwajibisha utendaji wa kaunti

Orodha ya Kaunti za Kenya

NambaKauntiMkoa wa zamaniEneo
(km2)
Wakazi
(Sensa 2009)
Makao Makuu
1Mombasa (Kaunti)Pwani212.5939,370Mombasa (Jiji)
2KwalePwani8,270.3649,931Kwale
3KilifiPwani12,245.91,109,735Kilifi
4Tana RiverPwani35,375.8240,075Hola
5LamuPwani6,497.7101,539Lamu
6Taita–TavetaPwani17,083.9284,657Mwatate
7Garissa Kaskazini-Mashariki45,720.2623,060Garissa
8Wajir Kaskazini-Mashariki55,840.6661,941Wajir
9Mandera Kaskazini-Mashariki25,797.71,025,756Mandera
10MarsabitMashariki66,923.1291,166Marsabit
11IsioloMashariki25,336.1143,294Isiolo
12MeruMashariki6,930.11,356,301Meru
13Tharaka-NithiMashariki2,409.5365,330Chuka
14EmbuMashariki2,555.9516,212Embu
15KituiMashariki24,385.11,012,709Kitui
16MachakosMashariki5,952.91,098,584Machakos
17MakueniMashariki8,008.9884,527Wote
18NyandaruaKati3,107.7596,268Ol Kalou
19NyeriKati2,361.0693,558Nyeri
20KirinyagaKati1,205.4528,054Kerugoya / Kutus
21Murang'aKati2,325.8942,581Murang'a
22KiambuKati2,449.21,623,282Kiambu
23Turkana Bonde la Ufa71,597.8855,399Lodwar
24West Pokot Bonde la Ufa8,418.2512,690Kapenguria
25Samburu Bonde la Ufa20,182.5223,947Maralal
26Trans-Nzoia Bonde la Ufa2,469.9818,757Kitale
27Uasin Gishu Bonde la Ufa2,955.3894,179Eldoret
28Elgeyo-Marakwet Bonde la Ufa3,049.7369,998Iten
29Nandi Bonde la Ufa2,884.5752,965Kapsabet
30Baringo Bonde la Ufa11,075.3555,561Kabarnet
31Laikipia Bonde la Ufa8,696.1399,227Rumuruti
32Nakuru Bonde la Ufa7,509.51,603,325Nakuru
33Narok Bonde la Ufa17,921.2850,920Narok
34Kajiado Bonde la Ufa21,292.7687,312Kajiado
35Kericho Bonde la Ufa2,454.5752,396Kericho
36Bomet Bonde la Ufa1,997.9730,129Bomet
37KakamegaMagharibi3,033.81,660,651Kakamega
38VihigaMagharibi531.3554,622Vihiga
39BungomaMagharibi2,206.91,375,063Bungoma
40BusiaMagharibi1,628.4743,946Busia
41SiayaNyanza2,496.1842,304Siaya
42KisumuNyanza2,009.5968,909Kisumu (Jiji)
43Homa BayNyanza3,154.7963,794Homa Bay
44MigoriNyanza2,586.4917,170Migori
45KisiiNyanza1,317.91,152,282Kisii
46NyamiraNyanza912.5598,252Nyamira
47Nairobi (Kaunti)Nairobi (Mkoa)694.93,138,369Nairobi (Jiji)
581,309.038,610,097Nairobi

Kazi ya Serikali

Serikali za kaunti zina wajibu wa kutunga sheria katika mabunge ya kaunti na utendaji katika kaunti. Kazi ya kaunti kulingana na kiambatisho cha nne cha katiba ni:

  1. Ukulima, ikiwa ni pamoja na:
    • mimea na ufugaji wa wanyama
    • maeneo ya uuzaji wa mifugo
    • vichinjio vya kaunti
    • udhibiti wa magonjwa ya wanyama na mimea
    • uvuvi
  2. Huduma za afya
    • vifaa vya afya vya kaunti na maduka ya dawa
    • huduma za ambulensi
    • ukuzaji wa huduma msingi za afya
    • utoaji leseni na udhibiti wa shughuli zinazohusu uuzaji wa vyakula kwa umma
    • huduma za afya ya mifugo
    • makaburi, mochari na vifaa vya uchomaji maiti
    • kuondoa taka na maeneo ya kutupia taka
  3. Udhibiti wa uchafuzi wa hewa, kelele, kero zinginezo kwa umma na matangazo ya nje
  4. Shughuli za kitamaduni, burudani za umma na maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na:
    • kamari, kasino na aina nyingineyo ya kamari
    • mbio
    • utoaji leseni za pombe
    • sinema
    • maonyesho ya video na ukodishaji wake
    • maktaba
    • makumbusho
    • shughuli za michezo na utamaduni na maeneo yake
    • bustani, fuko na maeneo ya starehe
  5. Usafiri katika kaunti, ikiwa ni pamoja na:
    • barabara za kaunti
    • mataa ya barabarani
    • trafiki na maegesho
    • usafiri wa umma barabarani
    • feri na bandari, isipokuwa udhibiti wa mambo yanayohusiana na usafiri wa meli wa kitaifa na kimataifa .
  6. Udhibiti wa wanyama na ustawi wao, ikiwa ni pamoja na:
    • kutoa leseni za mbwa
    • maeneo ya malazi, utunzaji na uzikaji wa wanyama
  7. Uendelezaji wa biashara na udhibiti wake, ikiwa ni pamoja na:
    • masoko
    • kutoa leseni za biashara (isipokuwa udhibiti wa wataalamu)
    • shughuli za biashara zilizo haki
    • utalii wa ndani kwa ndani
    • vyama vya ushirika
  8. Upangaji wa kaunti na uendelezaji, ikiwa ni pamoja na:
    • takwimu
    • usoroveya wa ardhi na uchoraji ramani
    • mipaka na nyua
    • makazi
    • maelekezo ya usambazaji wa umeme na gesi na udhibiti wa nishati
  9. Elimu ya chekechea, vyuo vya ufundi vijijini, vituo vya ufundi na maeneo ya malezi ya watoto
  10. Utekelezaji wa sera maalum za serikali ya kitaifa kuhusu raslimali za kiasili na uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:
    • uhifadhi wa udongo na maji
    • misitu
  11. Huduma za kaunti kwa umma, ikiwa ni pamoja na:
    • mifumo ya kudhibiti maji kutokana na kibunga
    • huduma za maji na usafi
  12. Huduma za zimamoto na udhibiti wa majanga
  13. Udhibiti wa dawa za kulevya na ponografia
  14. Kuhakikisha na kuratibu ushiriki wa jamii na kata katika utawala katika ngazi za mashinani na kusaidia jamii na kata zipate uwezo wa kitawala kwa sababu ya utekelezaji wenye ufanisi wa nguvu na kazi na ushiriki katika utawala katika ngazi za mashinani.

Marejeo