Kiswahili

Lugha ya Kibantu inayozungumzwa zaidi Afrika ya Mashariki

Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye misamiati mingi ya Kiarabu (35%[1]), lakini sasa ya Kiingereza pia (10%), inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki.

Maeneo yenye wasemaji wa Kiswahili.
Mfano wa kusema Kiswahili.

Lugha hii ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, methali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili hutumika kufundishia shuleni na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa kutumia lugha hiyo, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya au riwaya.

Historia ya lugha

Makala kuu ya: Historia ya Kiswahili
Kiswahili kilianza kuandikwa kwa herufi za Kiarabu pekee kwa karne nyingi: "Huu ni ukumbusho wa askari wenyeji Waafrika waliopigania katika Vita Kuu..." (Matini kwenye Sanamu ya Askari, Dar es Salaam).

Lugha ilianza takribani miaka 800-1000 iliyopita katika mazingira ya vituo vya biashara vya pwani ambako wafanyabiashara kutoka Uarabuni, Uajemi na Uhindi walikutana na wenyeji Waafrika. Lugha kuu ya kimataifa ya biashara hiyo ilikuwa Kiarabu.

Inaonekana ya kwamba lugha mpya ilijitokeza wakati wenyeji wa pwani, waliokuwa wasemaji wa lugha za Kibantu, walipopokea maneno mengi hasa ya Kiarabu katika mawasiliano yao. Kwa hiyo msingi wa Kiswahili ni sarufi na msamiati wa Kibantu pamoja na maneno mengi ya Kiarabu. Imekadiriwa ya kwamba karibu theluthi moja ya maneno ya Kiswahili yana asili ya Kiarabu.

Kando ya Kiarabu toka zamani pia kuna athira ya lugha mbalimbali kama Kiajemi, Kihindi na Kireno.

Kuanzia karne ya 20 hadi sasa maneno mengi yamepokewa kutoka Kiingereza, na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Kifaransa, lakini pia kutoka lugha nyingine, hasa Kiarabu.

Kwa karne nyingi iliandikwa kwa herufi za Kiarabu (سواحلي sawahili au لغة سواحيلية lugha sawahiliya).

Sarufi ya kwanza pamoja na kamusi iliandikwa mwaka 1848 na Dokta Ludwig Krapf huko Rabai Mpya / Mombasa.

Kiswahili kilikuwa na lahaja nyingi kutokana na lugha mbalimbali za Kibantu zilizochangia katika eneo husika.

Tangu karne ya 19 lugha ilianza kuenea barani kwa njia ya biashara.

Wakati wa ukoloni wa Uingereza lugha ilisanifishwa na Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili kwenye msingi wa lahaja ya Unguja.

Wasemaji

Kiswahili barani Afrika.

Hakuna hakika kuhusu idadi ya wasemaji wa lugha hiyo; idadi zinazotajwa zinatofautiana, lakini ni kati ya milioni 100 na 200 [2], kwa sababu wasemaji wanaoitumia kama lugha ya kwanza hawapungui milioni 20, na wasemaji wanaoitumia kama lugha ya pili ni zaidi ya milioni 90.

Tena idadi ya wasemaji wa lugha ya kwanza inakua haraka, kwa sababu lugha inaenea katika maeneo ambapo hapo awali lugha nyingine zilitawala; hasa katika miji ya Tanzania imekuwa lugha kuu, badala ya lugha za kikabila, kutokana na mchanganyiko wa watu hata ndani ya nyumba moja, kama vile wanapooana watu wa makabila tofauti, jambo ambalo limekuwa la kawaida hasa Tanzania, ambayo inaongoza kwa matumizi ya Kiswahili. Kwa watoto wengi kimekuwa lugha mama[3].

Kati ya nchi nyingine ambapo Kiswahili kinatumika kuna Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Somalia, Zambia, Malawi na visiwa vya Bahari Hindi kama Visiwa vya Ngazija (Komoro).

Lugha rasmi

Kiswahili kimekuwa lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, katika Umoja wa Afrika na katika nchi zifuatazo:

  • Kenya: ni lugha ya taifa tena lugha rasmi, sawa na Kiingereza, baada ya rasimu ya katiba mpya kupitishwa tarehe 4 Agosti 2010; Kiswahili ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kati ya wananchi wakikutana nje ya eneo lenye kabila moja tu; ni lugha inayofundishwa lakini si lugha ya kufundisha mashuleni; ni lugha inayotumika na polisi na jeshi, ni lugha ya kuhutubia wananchi mjini na kitaifa; sehemu za ibada makanisani zinatumia Kiswahili; kuna gazeti moja tu la Kiswahili; sehemu za programu redioni na kwenye runinga ni kwa Kiswahili. Hata hivyo, lugha inachanganywa mara nyingi na Kiingereza na lugha za maeneo au za kikabila.
  • Uganda: kimetangazwa kuwa lugha ya taifa tangu 2005; iliwahi kuwa lugha ya taifa wakati wa utawala wa Idi Amin; wakati wa ukoloni ilifundishwa mashuleni ikaelekea kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza lakini matumizi haya yalipingwa hasa na Waganda hivyo Waingereza waliacha mipango hiyo. Ni lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo imeleta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda; watu wengi bado hukumbuka hasa matusi ya wanajeshi waliowatesa wakisema Kiswahili. Lakini kuna maeneo ya Uganda ambako Kiswahili kinatumiwa na watu wengi kama lugha ya sokoni na barabarani. Wona UBC, WBS tv. Mwaka 2005 bunge lilipiga kura kukifanya lugha rasmi ya pili kwa kuwa kinazungumzwa zaidi (nje ya Buganda).

Lugha ya kwanza, lugha ya pili

Kiasili Kiswahili kilikuwa lugha ya kwanza tu ya wakazi wa miji ya Waswahili kwenye pwani, katika sehemu za pwani pia kijijini. Baada ya kuenea kimekuwa lugha ya watu wengi mjini hasa Tanzania lakini pia Kenya.

Kimeenea zaidi kama lugha ya mawasiliano na biashara pale ambako watu wa makabila mbalimbali wanakutana. Pamoja na nchi zinazotajwa hapo juu Kiswahili kinatumika Kaskazini mwa Msumbiji, Kusini kabisa ya Somalia, Mashariki mwa Burundi.

Maeneo ya mpaka wa Tanzania kuna pia wasemaji kadhaa huko Malawi na Zambia.

Tanzania na Kenya zilipokea wakimbizi wengi waliojifunza Kiswahili lakini hakuna uhakika kama bado kinatumiwa nao baada ya kurudi Afrika Kusini, Rwanda, Sudan Kusini, Somalia n.k.

Kimataifa

Radio France Internationale kwa Kiswahili.

Lugha hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa jumla, na hasa Afrika, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali, na kukusanya kwake watu wa makabila na nchi kadha wa kadha wakaweza kufahamiana kwa lugha moja, hasa ilivyokuwa ni lugha mojawapo katika lugha kubwa za Afrika ambazo zinachukuwa mahala pa lugha za kigeni na wakoloni, kama Kiarabu, Kiurdu, Kiebrania, Kireno na kadhalika.

Leo imekuwa inatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbalimbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche Welle, Monte Carlo, RFI, na nchi nyinginezo kama vile Uchina, Urusi, Irani.

Aidha, imekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani, Uingereza, Ulaya bara, Urusi, Uchina, na barani Afrika.

Mwaka 2018 Afrika Kusini ilikubali Kiswahili iweze kufundisha shuleni kama somo la hiari kuanzia mwaka 2020. Botswana ilifuata mwaka 2020, na Namibia ina mpango kama huo. Pia Ethiopia na Sudan Kusini zimeanza kufundisha Kiswahili.

Maendeleo ya Kiswahili

Lugha ina maendeleo: inaweza kukua, kukwama au kufa. Athira nyingi hutokea bila mpangilio pale ambako wasemaji wanapokea maneno mapya, wanaacha kutumia maneno mengine au hubadilisha kawaida ya matamshi au sarufi. Haya yote hutokea pia katika uwanja wa Kiswahili.

Kuna mzaha unaosimuliwa hasa Tanzania: Kiswahili kilizaliwa Unguja, kilikua Tanzania Bara, kikafa Kenya na kuzikwa Uganda. Hali halisi Kiswahili kina maendeleo yake katika nchi hizo zote labda zaidi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo matumizi yake ni kwa njia ya lahaja za Kingwana.

Lakini itategemea pia juhudi za serikali kama umoja wa lugha utatunzwa kwa sababu kuna athari nyingi kutoka lugha za kila eneo zinazoingia katika ukuzi wa Kiswahili kwa namna zinazotofauitiana.

Taasisi zinazokuza Kiswahili

Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu vingine vya Kenya na pia Uganda.

Nchini Tanzania kuna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ilhali nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). BAKITA na CHAKITA pamoja na wawakilishi kutoka Uganda wanaandaa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la Afrika Mashariki (BAKAMA).

Uchunguzi wa Kiswahili huendelea pia katika idara za vyuo vikuu vingi duniani, kwa mfano katika Institute National des Langues et Civilisations Orientales, jijini Paris, Ufaransa.

Kamusi za Kiswahili

Makala kuu ya: Kamusi za Kiswahili

Kati ya shughuli muhimu za taasisi hizo, mojawapo ni kazi ya kukuza misamiati ya Kiswahili yaani kutafuta maneno mapya au kupanua matumizi ya maneno yaliyopo ili kutaja mambo ya maisha ya kisasa yaliyobadilika. Utunzi wa kamusi za Kiswahili hupanua elimu hiyo.

Faida za kutumia Kiswahili kwa mataifa ya Afrika

Faida za kutumia lugha ya Kiswahili zinatajwa kama ifuatavyo:

  • 1. Husaidia kuleta umoja wa bara zima.
  • 2. Hudumisha utamaduni wa Kiafrika kuliko kufuata kasumba.
  • 3. Hufanya Waafrika waamini zaidi mambo yao kuliko kutegemea tu ya kigeni.
  • 4. Hurahisisha mawasiliano baina ya watu wa Afrika Mashariki.
  • 5. Husaidia kuwa na mahusiano ya kibiashara na watu mbalimbali.
  • 6. Ni ishara ya kuwa huru na kushikamana.
  • 7. Ni utambulisho wa jamii husika (utaifa).
  • 8. Husaidia kukuza na kuendeleza sanaa.
  • 9. Husaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika taifa husika.
  • 10. Husaidia kupata ajira katika vyuo na shule mbalimbali zinazofundisha lugha ya Kiswahili hata nje ya nchi.
  • 11. Husaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wa lugha hiyo watakaofanya vizuri katika masomo kwa kuyaelewa zaidi.
  • 12. Husaidia kuikuza na kuieneza ndani na nje ya jamii.

Mengineyo

Siku ya Kiswahili Duniani ilianzishwa na UNESCO mnamo mwaka 2021 ili kuadhimishwa kila tarehe 7 Julai kuanzia mwaka 2022[4]. Tarehe hiyo imechaguliwa kwa sababu ndipo Julius Kambarage Nyerere alipochagua kutumia lugha hiyo katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Tazama pia

Tanbihi

Marejeo

  • Ashton, E. O. 1944. Swahili Grammar (Including Intonation). London: Longmans.
  • Hinnebusch, T. J. 1979. "Swahili". Katika: T. Shopen (mhariri) Languages and Their Status, uk. 209-293. Cambridge, Massachusetts: Winthrop.
  • Hinnebusch, T. J., and S. M. Mirza. 1979. Kiswahili: Msingi wa Kusema, Kusoma na Kuandika. Lanham, MD: University Press of America.
  • Shihabdin Chiraghdin et Mathias E. Mnyampala. Historia ya Kiswahili. Oxford University Press, 1977.
  • Nurse, D. and Hinnebusch, T. J. 1993. Swahili and Sabaki: A Linguistic History. Berkeley and Los Angeles: University of California Press.
  • Ohly, Rajmund, Warsaw: Wydawnictwa Uniwersytetu warszawskiego,
    • Język suahili,
      • Ⅰ. Zarys gramatyki ⅠⅠ. Wybór tekstów, 1969 ;
      • Teksty suahili w piśmie arabskim wraz z ćwiczeniami i wprowadzeniem metodologicznym, 1972,
    • Literatura suahili, 1972.
  • Ohly, R., Kraska-Szlenk, I., and Podobińska, Z., Język suahili, Warsaw: Wydawnictwo Akademickie Dialog, 1998.
  • Wald, B. 1987. "Swahili and the Bantu Languages". Katika: B. Comrie (mhariri) The World's Major Languages, uk. 991-1014. New York: Oxford University Press.
  • Whiteley, W. 1969. Swahili: The Rise of a National Language. London: Methuen.
  • Zawawi, S. 1971. Kiswahili Kwa Kitendo: An Introductory Course. New York: Harper & Row.

Viungo vya nje