Moroko (pia Maroko, kwa Kiarabu المغرب), au kirefu Ufalme wa Moroko (المملكة المغربية al-mamlaka al-maghribiya yaani "ufalme wa magharibi") ni nchi ya Afrika ya Kaskazini-Magharibi.
Maeneo ya Kihispania ya Ceuta na Melilla yamezungukwa na Moroko kwenye pwani ya Mediteranea.
Mpaka wa kusini haueleweki vizuri kwa sababu Moroko inadai ya kwamba Sahara ya Magharibi ni sehemu ya eneo lake, hali isiyokubaliwa na jumuiya ya kimataifa tangu Moroko ilipovamia Sahara ya Kusini mwaka 1975.
Eneo la Moroko ni km² 446,550. Sehemu kubwa ni jangwa la Sahara. Watu walio wengi huishi kwenye sehemu za rutuba karibu na pwani.
Kuna milima inayofunika maeneo makubwa. Milima ya Rif inaongozana na pwani ya Mediteranea yenye mwelekeo kutoka kaskazini-magharibi kwenda kaskazini-mashariki. Milima ya Atlas iko katikati ya nchi kutoka kusini-magharibi kwenda kaskazini-mashariki.
Miji mikubwa
Mji mkuu ni Rabat wenye wakazi milioni 1.2. Mji mkubwa ni Casablanca (kwa Kiarabu: الدار البيضاء dar al-baiDa = nyumba nyeupe). Miji yote miwili mikubwa ni miji ya bandari.
Miji mitano mikubwa ni kama ifuatavyo (namba za sensa ya mwaka 2004):
Habari za kimaandishi za kwanza ni kutoka karne za kwanza KK. Wafinisia walijenga miji yao pwani lakini eneo la ndani lilibaki nchi ya Waberber waliounda ufalme wa Mauretania ya Kale (usiuchanganye na nchi ya kisasa Mauretania) uliounganisha sehemu kubwa ya Moroko ya kaskazini.
Wamauretania wa kale walishirikiana na Dola la Roma hadi kuwa jimbo la dola hili kwa jina la "Mauretania Tingitana".
Wakati wa kudhoofika kwa Dola la Roma kuanzia mwaka 400BK kukawa na uvamizi wa Wavandali.
Mwanzoni Moroko ilikuwa sehemu ya milki ya khalifa ya Waomawiyya waliotawala Dameski (Siria). Baada ya kupinduliwa kwa Waomawiyya na Waabasiya wa Baghdad (Iraq) mkimbizi Mwarabu Idris ibn Abdallah (788-791) alikusanya makabila ya Waberber na kuunda milki ya kujitegemea. Hii ilikuwa mwanzo wa Moroko kuwa milki ya Kiislamu inayojitawala.
Watawala wa kienyeji
Vipindi vya historia husebabiwa kufuatana na familia zilizofuatana za wafalme Waarabu au Waberber.
Wamuwahidun waliendelea kupanuka kuelekea Misri lakini baadaye walidhoofika wakapaswa kuwaachia Wahispania Wakristo sehemu za Andalusia. Athira ya milki ya Moroko ilipungua baadaye hadi Hispania yote ikarudishwa kwa watawala Wakristo mwaka 1492; pia utawala kusini kwa Sahara haukuendelea.
Wareno wa Wahispania waliendelea kuteka miji kwenye pwani za Moroko. Utawala wa Hispania juu ya Ceuta na Melilla leo ni mabaki ya nyakati zile.
Sehemu za nchi zilianza kujitawala bila kukubali tena mamlaka wa juu, kwa mfano makabila ya Waberber milimani au miji ya Rabat na Sale iliyounda dola dogo la Jamhuri ya Bou Regreg katika karne ya 17 na kujishughulisha na uharamia.
Katika karne ya 17familia ya Waalawi walishika mamlaka wakaendelea nayo hadi leo. Waliweza kutunza uhuru wa nchi hadi mwanzo wa karne ya 20. Lakini mwanzo wa karne ya 20 Ufaransa na Hispania walimlazimisha mfalme Mulay Abdelaziz kukubali mkataba uliofanya Moroko kuwa kama koloni chini ya nchi hizo mbili.
Baada ya vita Wafaransa walijaribu kukandamiza mwendo huo wakamwondoa Sultani Mohammed V nchini 1953. Ghasia zikaongezeka, Sultani akarudi na nchi ikapewa uhuru mwaka 1956.
Utawala wa mwanae Hassan II kuanzia mwaka 1961 uliitwa "miaka ya risasi" kwa sababu mfalme alikataa kukubali utaratibu wa kidemokrasia. Chaguzi zilikuwa za uwongo, wapinzani wakatupwa jela au kuuawa. Hassan II alishinda majaribio mbalimbali ya kumpindua. Siasa ya kushikamana na Marekani ilimsaidia mfalme kimataifa lakini baada ya mwisho wa "vita baridi" alilazimishwa na Wamarekani kulegeza utawala wake.
Kaskazini mwa nchi ambako kitovu chake ni Fes kuna zaidi tabia ya Kiarabu, wakatu kusini ambako kitovu chake ni Marakesh kuna tabia ya Kiberber zaidi.
Lugha
Lugha rasmi ya nchi ni Kiarabu na Kiberberi. Waberber wengi, hasa kaskazini, wameacha lugha yao na kutumia Kiarabu lakini walileta maneno yao katika lahaja ya Kiarabu cha Kimaroko. Hata Kifaransa kinatumika sana.
Dini
Uislamu ndio dini rasmi na ndio unaofuatwa na wakazi wengi sana (98.9%), hasa Wasunni. Wengine ni Wakristo (0.9%) na Wayahudi (0.2%). Wakristo karibu wote ni wa asili ya Ulaya. Wayahudi waliwahi kuwa wengi kidogo, lakini idadi yao imepungua katika miaka ya nyuma kutokana na uhamaji hata kama hali yao katika taifa ni nzuri kulingana na nchi nyingine za Kiarabu.
Uchumi
Nguzo za uchumi wa nchi ni kilimo na magodi ya kuchimba madini, pamoja na uvuvi na utalii.
Zaidi ya asilimia 40 za wananchi hulima. Kwa jumla asilimia 18 za eneo la Moroko zinatumiwa kwa kilimo, hasa katika magharibi na kaskazini-magharibi.
Nchi hii ina akiba kubwa ya fosfati inayochimbwa na kuuzwa nje kwa matumzi ya mbolea. Akiba ya fosfati ni kubwa duniani. Moroko ina nafasi ya tatu katika uzalishaji baada ya China na Marekani[1].
Umuhimu wa utalii kwa uchumi umezidi kukua; mwaka 2018 idadi ya watalii ilifikia milioni 12.3[2]Vivutio vya kitalii ni pamoja na mahali pa urithi wa dunia kama vile
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Moroko kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.