Dajaja (kundinyota)

Dajaja (kwa Kilatini na Kiingereza Cygnus) [1] ni jina la kundinyota kwenye angakaskazi ya Dunia yetu. Humo ipo Dhanabu ya Dajaja (Deneb)[2] ambayo ni kati ya nyota angavu zaidi kwenye anga ya usiku na hii ni nyota moja ya Pembetatu ya Kiangazi kwenye angakaskazi.

Nyota za kundinyota Dajaja (Cygnus) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Dajaja - Cygnus jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji wa angakaskazi

Nyota za α - β na ε - δ zimelinganishwa na umbo la msalaba na hivyo zinaitwa pia "Salibu ya Kaskazini".

Jina

Dajaja (Cygnus) ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu wanaosema الدجاجة ad-dajaaja wakimtaja ndege wa aina ya kuku. [3]. Waarabu walipokea jina hili kutoka kwa Ptolemaio aliyeiita Ορνις ornis yaani ndege au kuku[4]. Wagiriki wa Kale kwa jumla waliona hapa ndege waliotaja kwa majina tofauti[5] .

Katika mapokeo ya baadaye hasa wakati wa Kiroma ndege ilichukuliwa kumaanisha bata-maji au “kyknos” (lat. Cygnus) iliyounganishwa na ndege huyu wa angani kati ya Wagiriki na Waroma wa Kale. Katika mitholojia ya Kigiriki "kyknos"inaweza kurejelea masimulizi ya mungu mkuu Zeus aliyechukua umbo la bata maji akitembea duniani na kutafuta mapenzi na mabinti wa kibinadamu[6]. Kwa mapokeo tofauti jina la “kyknos” linarejelea masimulizi ya mungu Phaeton aliyekuwa mwana wa Helios mungu wa jua. Phaeton aliwahi kuendesha gari la jua la babaye angani kwa kasi kubwa mno akasababisha hatari ya kuchomwa kwa mbingu na Dunia. Hapo baba wa miungu Zeus alipaswa kurusha radi dhidi ya gari la jua na kumwua Phaeton. Phaeton akaanguka chini katika mto Nahari (Eridanus) na kwa muda mrefu rafiki yake Kyknos alitafuta mifupa yake katika vilindi vya mto ili aweze kumpatia mazishi halisi. Miugu kwa jumla waliguswa na upendo alionyesha wakamgeuza kuwa kyknos = bata-maji na kumweka angani kati ya nyota. Kwa hiyo Waarabu walitumia hapa jina la kale zaidi la Wagiriki kwa kundinyota hili. Katika mapokeo ya kimagharibi kuna pia mifano ambako “Gallina” (=Kuku) ilitumiwa badala ya Cygnus hadi karne ya 18.[7].

Cygnus - Dajaja ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio (kwake kama ornis - ndege) katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [8] kwa jina la Cygnus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Cyg'.[9]

Mahali pake

Dajaja - Cygnus inaonekana katika kanda ya Njia Nyeupe. Inapakana na kundinyota jirani za Kifausi (Cepheus), Tinini (Draco), Kinubi (Lyra), Farasi (Pegasus), Mjusi (Lacerta) na Mbweha (Vulpecula)

Nyota

Dhanabu ya Dajaja[10] au α Cygni (Deneb) ni nyota angavu zaidi. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 1.25; umbali wake na Dunia bado unajadiliwa kuna makadirio kati ya miakanuru 1,425 hadi 3,200[11][12].


Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
α50Deneb (Dhanabu ya Dajaja)1,25m3200A2 Ia
γ37Sadr2,23m750F8
ε53Gienah2,48m72K0 III
β6Albireo2,9m385K2 + B9 V
δ182,86m150B9 + F1
343,0 bis 6,0m5000B2 Ia
ζ643,21m200G8 III
χ3,62 bis 15,0m345K0 III
ξ623,72m1000K5 Ib
τ653,74m70F1 IV
ι103,76m100A5 V
κ13,80m150K0 III
ο1313,80m500K2 + B6
η213,89m200K0 III
ν583,94m150A0 V
ο2323,96m1000K3 ib
ρ733,98m200G8 III
414,01m500F5 II
6161 Cygni4.8m11.4K5 + K7
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Argo Navis” ukurasa 374 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Paul Kunitzsch: Der Almagest: die Syntaxis mathematica des Claudius Ptolemäus in arab. -latein. Überlieferung, Otto Harrassowitz Verlag, 1974, kisehemu online hapa kwa google books, uk. 179
  • PAL - Glossary, tovuti ya mradi wa "Ptolemaeus Arabus et Latinus (PAL)" wa Bavarian Academy of Sciences and Humanities, iliangaliwa Oktoba 2017