Katibu Mkuu

Katibu Mkuu ni cheo cha kiongozi katika chama, shirika, kanisa, klabu au taasisi. Kwa mujibu wa itifaki, yuko chini ya mkuu au mwenyekiti wa shirika, lakini mara nyingi ushawishi wake ni mkubwa kuliko wa yule ambaye ni kiongozi mkuu kwa jina. Kwa kawaida yeye ni mjumbe wa bodi kuu ya shirika, ndiye mkuu wa utawala katika shirika na mkuu wa wafanyakazi.

Kama shirika linaongozwa na kamati au bodi inayofanya maazimio ya msingi, Katibu Mkuu huwajibika kwa shughuli za kila siku.

Umoja wa Mataifa

Katika Umoja wa Mataifa cheo cha Katibu Mkuu wa UM kinamtaja mtendaji kiongozi wa ofisi kuu.

Serikali na wizara

Katika nchi nyingi kiongozi wa utawala ndani ya wizara fulani huitwa Katibu Mkuu akifanya kazi chini ya waziri ambaye ni kiongozi wa kisiasa. Ilhali mawaziri hubadilishwa mara kwa mara, watumishi wa wizara hudumu na katibu mkuu ana kazi ya kuwasimamia na kupanga kazi yao.

Vyama vya Kikomunisti

Katika vyama vya Kikomunisti vilivyofuata mfumo wa Umoja wa Kisovyeti, katibu mkuu aliunganisha madaraka ya mwenyekiti na kiongozi wa utawala; mfumo huo ulianzishwa na Josef Stalin, kuendelezwa hata baada yake na kuigwa na vyama vingine. Hadi leo kiongozi wa chama cha Kikomunisti katika China, Vietnam, Laos, Korea Kaskazini na Kuba anatumia cheo cha katibu mkuu au "katibu wa kwanza" na kutokana na mfumo wa utawala ndiye pia kiongozi mwenye madaraka makuu katika nchi.

Cheo rasmiMwenye cheotangu
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha ChinaXi Jinping15 Novemba 2012
Katibu wa Kwanza wa Chama cha Wafanyakazi wa KoreaKim Jong Un17 Desemba 2011
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha VietnamNguyễn Phu Trọng19 Januari 2011
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi cha Wananchi wa LaosThongloun Sisoulith15 Januari 2021
Katibu wa Kwanza wa Chama cha Kikomunisti cha KubaMiguel Diaz-Canel19 Aprili 2021