Muungano wa Kijerumani

Muungano wa Kijerumani ( Kijerumani : Deutsche Wiedervereinigung , Kiing. German Reunification) ulikuwa mchakato wa kuunganisha sehemu za Ujeruamni zilizowahi kutenganishwa. Muungano huo ulitokea kwenye mwaka 1990 wakati majimbo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (Ujerumani Mashariki) yalijiunga na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani (Ujerumani Magharibi).

Mgawanyiko wa Ujerumani, 1949. Ujerumani Magharibi (bluu) ina Kanda za Amerika, Uingereza na Ufaransa (bila Saar), Ujerumani Mashariki (nyekundu) huundwa kutoka kwa Ukanda wa Soviet.

Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Ujerumani iligawanywa na washindi kwa kanda nne vilivyosimamiwa na Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa.

1949 Wajerumani walianza tena kujitawala katika nchi mbili. Kanda za Marekani, Uingereza na Ufaransa ziliungana kwa jina la Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani liliofuata siasa ya demokrasia ya vyama vingi na uchumi wa kibepari. Kanda la Kirusi lilikuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani lililofuata siasa ya utawala wa chama cha kikomunisti na uchumi wa kijamaa.

Hadi mwaka 1960 uchumi wa magharibi umepita ule wa mashariki. Hali ya maisha katika magharibi ilianza kuwa bora na pamoja na udikteta wa kisiasa wa Wakomunisti wananchi wengi wa mashariki walivuka mpaka wakahamia magharibi. Kwa hivyo serikali ya mashariki ilianza kujenga fensi kwenye mpaka na kwenye Agosti 1961 ilijenga ukuta wa Berlin uliozuia watu wa mashariki wasiweze tena kufika magharibi.

Hadi mwaka 1989 hali ya kiuchumi katika mashariki ilizidi kubaki nyuma ya magharibi, na kwa jumla uchumi ulikuwa matatani. Wakati ule kiongozi wa Umoja wa Kisoveti Mikhail Gorbachev alianza kulegeza ukali wa utawala wa kikomunisti[1] . Watu wengi kwenye mashariki hawakuwa tena tayari kunyamaza na idadi ya wakimbizi wa kwenda magharibi iliongezeka kwa ghafla wakipita nchi jirani za kikomunisti kama Chekoslovakia na Hungaria ambako watawala hawakuwa tayari tena kuwazuia[2] [3]. Wakati ule, Wajerumani wengi hawakuamini bado kwamba nchi itaunganishwa tena.[4]

Hatimaye mpaka ulifunguliwa tarehe 9 Novemba 1989[5]. Utawala wa Wakomunisti uliporomoka haraka na katika kipindi cha miezi 11 iliyofuata[6], masharti ya muungano yalijadiliwa kati ya Ujerumani Mashariki na Magharibi, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Umoja wa Kisovieti.

Mkataba wa Masuluhisho ya Mwisho kuhusu Ujerumani uliotiwa saini na nchi hizo mbili ndani ya Ujerumani na nchi za washindi wa Vita Kuu ulifungua njia kuelekea kuungana tena[7][8][9].

Tarehe 3 Oktoba 1990, saa 00:01 majimbo matano ya Brandenburg, Mecklenburg-Vorpommern, Saxony, Saxony-Anhalt, Thuringia na Berlin yalijiunga rasmi na Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani ilikoma kuwepo wakati huu.

Marejeo

Viungo vya Nje