Sepsisi

Sepsisi ni inflamesheni ya mwili mzima inayosababishwa na maambukizi.[1] Ishara na dalili zinazotokea mara nyingi zinajumuisha homa, kuongezeka kwa mdundo wa moyo, kuongezeka kwa kasi ya kupumua, na kuchanganyikiwa.[2] Kunaweza pia kuwa na dalili zinazohusiana na maambukizi maalum kama vile kukohoa pamoja na numonia au maumivu wakati wa kukojoa, na maambukizi ya figo. Watoto wachanga zaidi, wazee na watu wenye mfumo dhaifu wa kingamwili huenda wasiwe na dalili za maambukizi maalum na halijoto ya mwili huenda ikawa chini au kuwa ya kawaida wala si ya juu.[3] Sepsisi kali ni sepsisi inayosababisha utendakazi duni wa viungo au mtiririko usiotosha wa damu. Mtiririko usiotosha wa damu unaweza kudhihirika katika shinikizo la chini la damu, viwango vya juu vya lakteti kwenye damu, au uzalishaji wa chini wa mkojo. Mshtuko wa unaosababishwa na maambukizi ni shinikizo la chini la damu kutokana na maambukizi yasiyopungua hata baada ya kuongezwa viowevu vya kutosha kwa vena.[1]

Sepsisi
Mwainisho na taarifa za nje
SpecialtyInfectious diseases Edit this on Wikidata
ICD-10A40. – A41.
ICD-9995.91
DiseasesDB11960
MedlinePlus000666
MeSHD018805

Kisababishi na utambuzi

Sepsisi husababishwa na mwitikio wa kinga unaochochewa na maambukizi.[3][4] Maambukizi haya mara nyingi husababishwa na bakteria, lakini pia yanaweza kusababishwa na kuvu, virusi, au vimelea.[3] Viungo vinavyoathiriwa na maambukizi makuu mara nyingi vinajumuisha: mapafu, ubongo, kibofu cha mkojo, ngozi na viungo vya fumbatio. Vipengele vya hatari vinajumuisha umri mchanga au uzee, mfumo wa kinga uliodhoofishwa na hali kama vile saratani au kisukari, na jeraha kuu au maunguzo.[2] Utambuzi hutegemea kutimiza angalau vigezo viwili vya sindromu ya kimfumo ya mwitikio wa inflamesheni (SIRS) kutokana na maambukizi tarajiwa. Uchunguzi wa damu hupendekezwa ikiwezekana kabla ya kuanza kutumia antibiotiki; hata hivyo maambukizi ya damu si muhimu ili kudhibitisha ugonjwa huu.[3] Upigaji picha za kimatibabu unapaswa kufanywa ili kufahamu eneo la maambukizi.[1] Visababishi vingine vinavyoweza kusababisha ishara na dalili sawa na hizi zinajumuisha: anafilaksisi, kushindwa kwa utendakazi wa tezi za adrenali, kiasi cha chini cha damu, kushisndwa kwa moyo, na uemboli wa mapafu na kadhalika .[3]

Matibabu

Sepsisi kwa kawaida hutibiwa kwa viowevu vinavyodungwa kwenye mishipa na antibiotiki. Hii mara nyingi hufanywa katika kitengo cha wagonjwa mahututi. Ikiwa kuongezwa viowevu hakuimarishi shinikizo la damu, dawa za kuongeza shinikizo la damu zinaweza kutumika. Usambazaji wa hewa safi kutumia neli na dialisisi zinaweza kuhitajika ili kuboresha utendakazi wa mapafu na figo mtawalia.[2] Ili kuongoza matibabu, katheta ya mshipa wa kati wa vena na katheta ya ateri zinaweza kuwekwa. Vipimo vingine kama vile kiasi cha damu kinachotoka kwenye moyo na vena kava ya juu kukolea kwa oksijeni pia inaweza kutumika. Watu wenye maambukizi wanahitaji hatua za kinga dhidi ya thrombosisi ya mishipa ya ndani, vidonda kutokana na mfadhaiko na vidonda kutokana na shinikizo,isipokuwa ikiwa hali zingine zinazuia hatua kama hizi. Wengine wanaweza kufaidika kutokana na udhibiti mkali wa viwango vya sukari ya damu kwa kutumia insulini.[1] Matumizi ya kotikosteroidi yana utata.[5] Drotrecoginalfa iliyochochewa ambayo awali ilitumika katika maambukizi makali haijadhihirika kuwa bora hivyo iliachwa kuuzwa mwaka wa 2011.[6]

Prognosisi, epidemiolojia na historia

Wakati mwingine matokeo ya ugonjwa huu hutegemea ukali wake, huku hatari ya kifo kutokana na maambukizi ikiwa juu kwa asilimia 30, maambukizi makali yakiwa juu kwa asilimia 50 na mshtuko wa maambukizi ukiwa juu kwa asilimia 80.[7] Idadi jumla ya visa ulimwenguni kote haijulikani kwani kuna data kidogo kutoka kwa nchi zinazoendelea.[7] Makadirio yanaonyesha kuwa sepsisi inawaathiri mamilioni ya watu kila mwaka.[1] Katika nchi zilizoendelea takriban watu 0.2 hadi 0.3 kwa kila watu 1000 hupata sepsisi kila mwaka au takriban visa milioni moja kila mwaka nchini Marekani.[7][8] Kiwango cha kutokea kwa ugonjwa huu kimezidi kuongezeka.[1] Sepsisi hutokea zaidi katika wanaume kuliko kwa wanawake.[3] Maneno septikemia na sumu ya damu yanayoashiria viumbehai vidogo au toksini zake katika damu hayatumiki mara nyingi kwa sasa.[9][10] Maelezo ya hali hii yamekuwa yakitolewa angalau kuanzia nyakati za Hippocrates.[10]

Marejeleo