Musa Mwafrika

Musa Mwafrika, maarufu pia kama Musa Mwizi (330405), alikuwa mmonaki padri nchini Misri na mmojawapo kati ya mababu wa jangwani.

Mt. Musa Mwafrika.

Tangu kale anaheshimiwa na Wakristo wa madhehebu mengi kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 1 Julai katika Ukristo wa Mashariki na tarehe 28 Agosti katika Ukristo wa Magharibi[1].

Maisha

Mzaliwa wa Ethiopia[2], Musa alikuwa mtumishi wa afisa wa serikali nchini Misri mpaka alipofukuzwa kwa thuhuma za kuiba na kuua.[3]

Akiwa jitu, akawa bosi wa kundi la majambazi lililotisha watu wa bonde la Nile kwa ukatili.

Alipojaribu kukwepa waliokuwa wanamwinda, alifichama kwa wamonaki wa jangwani huko Wadi El Natrun (Sketes), karibu na Alexandria. Juhudi za kiroho, utulivu na furaha walivyokuwa navyo vilimuathiri kwa dhati. Muda mfupi baadaye aliacha mtindo wake wa kuishi, akabatizwa na kujiunga na monasteri ile.[4]

Kwanza alipata shida sana kuzoea nidhamu ya jumuia ile. Alipovamiwa na wezi chumbani mwake, aliwazidi nguvu akawaburuza hadi katika kikanisa walimokuwemo wenzake wakisali ili aambiwe awafanyie nini wageni hao.

Musa alikuwa na ari katika yote aliyoyafanya, lakini alikata tamaa alipojitambua si mkamilifu kutosha. Hapo abati Isidori alimchukua alfajiri hadi juu ya paa ili kutazama miali ya kwanza ya jua. Halafu akamuambia, "Taratibu tu miali ya jua inaondoa usiku na kuleta mchana mpya, na vilevile taratibu tu mtu anakuwa mwanasala kamili."[3]

Baadaye Musa akawa mwenyewe kiongozi wa jumuia ya wakaapweke katika sehemu nyingine ya jangwa akapewa upadrisho.[3]

Alipokuwa na umri wa miaka 75 hivi, ilisikika kwamba kundi la Waberber limepanga kushambulia monasteri yao. Wenzake walitaka kujihami, lakini Musa aliwazuia akawaambia ni afadhali wakimbie kuliko kushika silaha. Mwenyewe na wengine 7 walibaki hadi walipouawa tarehe 1 Julai.[4][5]

Kwa sababu hiyo Musa Mwafrika anaheshimiwa leo kama mtetezi wa msimamo wa kukataa silaha katika kudai haki.[6]

Tazama pia

Tanbihi

Marejeo

Viungo vya nje

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.