Pasaka ya Kiyahudi

Pasaka ya Kiyahudi (pia Passah au Pessah; Kiing. Passover) ni kati ya sikukuu muhimu zaidi za dini ya Uyahudi. Sikukuu hiyo inakumbuka Wanaisraeli walivyotoka katika utumwa walimokuwemo huko Misri.

Meza ya Seder yaani Chakula cha Pasaka ya Kiyahudi ikionyesha vitabu vya Haggada.
Sahani ya Seder ya Pasaka ya Kiyahudi.

Pasaka ya Kiyahudi imekuwa na athira kubwa juu ya sherehe ya Pasaka ya Kikristo kuhusu tarehe, liturujia na desturi mbalimbali.

Jina la Pasaka

Jina la Pasaka limetokana na neno la Kiebrania "פסח" (tamka: pasakh) lenye maana ya "kupita juu, kukaa juu ya (kama mlinzi)" katika kitabu cha Biblia cha Kutoka 12:23. Humo imeandikwa ya kwamba Mungu "atapita" juu ya milango ya nyumba za Wanaisraeli huko Misri katika usiku kabla ya kutoka kwao, na kuzuia maovu ambayo Wamisri waliathiriwa nayo.

Tarehe ya Pasaka ya Kiyahudi

Pasaka ina tarehe kamili katika kalenda ya Kiyahudi: inaanza 15 Nisan na kusheherekewa kwa siku saba hadi 22 Nisan. Siku ya kwanza na ya mwisho ni sikukuu hasa. Katika nchi ya Israel siku hizi mbili ni siku za kupumzika kazi. Wayahudi wengine, hasa nje ya Israel, husheherekea siku 8.

Kwa sababu kalenda ya Kiyahudi ni kalenda ya mwezi tarehe zake hubadilika katika hesabu ya kalenda ya Gregori yaani kalenda ya kawaida ya kimataifa. Kwa jumla Pasaka ya Kiyahudi inasheherekewa wakati wa miezi Machi au Aprili kwa sababu Nisan ni mwezi wa kwanza wa majira ya kuchipua.

Asili ya Pasaka

Katika Biblia, kitabu cha Kutoka, sura ya 12, kuna taarifa juu ya kutoka kwa Wayahudi katika Misri wakati wa Musa mnamo mwaka 1200 KK.

Taarifa ni kwamba Musa alitumwa na Mungu kuwaondoa Wanaisraeli katika hali ya utumwa huko Misri na kuwaongoza kwenda nchi ya ahadi. Lakini mfalme wa Misri mwenye cheo cha Farao alikataa, hivyo Mungu alituma mapigo dhidi ya Misri ili Farao alazimishwe kukubali.

Pigo la mwisho tena kali mno lilikuwa kifo cha kila aliyezaliwa kama mtoto wa kiume wa kwanza katika Misri. Hapo Wanaisraeli waliambiwa kuchinja mwanakondoo na kupaka damu yake milangoni kwao ili malaika akipita kuua watoto wa kwanza asiguse watoto wa Wanaisraeli.

Baada ya pigo hilo Farao alikubali Wanaisraeli watoke.

Tendo hilo la kuwaweka mababu yao huru linakumbukwa na Wayahudi kote duniani katika siku zinazoanza 15 Nisan.

Sherehe ya Pasaka

Sherehe ya Pasaka inaanza masaa ya jioni kabla ya siku yenyewe, kwa sababu katika kalenda ya Kiyahudi mwanzo wa siku si usiku kati wala macheo bali wakati wa machweo jioni inayotangulia.

Maandalizi ya sikukuu ni pamoja na kufanya usafi mkubwa kabisa katika nyumba. Hakuna kitu kilichochachuka kinachobaki katika nyumba kufuatana na Kutoka 12:20, yaani kitu chochote chenye nafaka au unga wake ulioguswa na maji, hata punje yake kama vile mkate, keki au spagetti. Tendo hili ni la kukumbuka jinsi Wanaisraeli walipaswa kukimbia Misri haraka bila muda wa kutengeneza mikate ya kawaida yaliyochachuka. Kwa hiyo wanawake wao walioka mikate yasiyochachuka ambayo yamekuwa chakula cha Pasaka hadi leo. Mikate hii huitwa "matze".

Familia na marafiki hukutana kwa chakula cha pekee wakizunguka meza ya Seder (seder = "utaratibu") yenye vyakula vya pekee.

Kati ya vyakula hivyo, mboga chungu inakumbusha uchungu wa utumwa, matunda ya kupondwa yenye rangi ya kahawia-nyekundu yanakumbusha udongo wa matofali ambayo Wanaisraeli walipaswa kutengeneza, maji ya chumvi yanakumbusha machozi huko Misri, mayai ni ishara ya matumaini, na vingine.

Vyote huliwa katika utaratibu (=seder) maalumu pamoja na masomo na sala kutoka vitabu vya Haggada vinavyoshikwa na wote mezani.

Tarehe za Pasaka ya Kiyahudi (Passa) katika Kalenda ya Gregori 2005 - 2050
Mwaka wa Kalenda ya GregoriMwaka wa Kalenda ya kiyahudiTarehe ya Pasaka huko IsraelTarehe ya Pasaka kwa Wayahudi wa Kiorthodoksi nje ya Israel
200457646-12 Aprili6-13 Aprili
2005576524-30 Aprili24 Aprili-1 Mei
2006576613-19 Aprili13-20 Aprili
200757673-9 Aprili3-10 Aprili
2008576820-26 Aprili20-27 Aprili
200957699-15 Aprili9-16 Aprili
201057705-11 Aprili5-12 Aprili
2011577119-25 Aprili19-26 Aprili
201257727-13 Aprili7-14 Aprili
2013577326 Machi-1 Aprili26 Machi-2 Aprili
2014577415-21 Aprili15-22 Aprili
201557754-10 Aprili4-11 Aprili
2016577623-29 Aprili23-30 Aprili
2017577711-17 Aprili11-18 Aprili
2018577831 Machi-6 Aprili31 Machi-7 Aprili
2019577920-26 Aprili20-27 Aprili
202057809-15 Aprili9-16 Aprili
2021578128 Machi-3 Aprili28 Machi-4 Aprili
2022578216-22 Aprili16-23 Aprili
202357836-12 Aprili6-13 Aprili
2024578423-29 Aprili23-30 Aprili
2025578513-19 Aprili13-20 Aprili
202657862-8 Aprili2-9 Aprili
2027578722-28 Aprili22-29 Aprili
2028578811-17 Aprili11-18 Aprili
2029578931 Machi-6 Aprili31 Machi-7 Aprili
2030579018-24 Aprili18-25 Aprili
203157918-14 Aprili8-15 Aprili
2032579227 Machi-2 Aprili27 Machi-3 Aprili
2033579314-20 Aprili14-21 Aprili
203457944-10 Aprili4-11 Aprili
2035579524-30 Aprili24 Aprili-1 Mei
2036579612-18 Aprili12-19 Aprili
2037579731 Machi-6 Aprili31 Machi-7 Aprili
2038579820-26 Aprili20-27 Aprili
203957999-15 Aprili9-16 Aprili
2040580029 Machi-4 Aprili29 Machi-5 Aprili
2041580116-22 Aprili16-23 Aprili
204258025-11 Aprili5-12 Aprili
2043580325 Aprili-1 Mei25 Aprili-2 Mei
2044580412-18 Aprili12-19 Aprili
204558052-8 Aprili2-9 Aprili
2046580621-27 Aprili21-28 Aprili
2047580711-17 Aprili11-18 Aprili
2048580829 Machi-4 Aprili29 Machi-5 Aprili
2049580917-23 Aprili17-24 Aprili
205058107-13 Aprili7-14 Aprili
Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pasaka ya Kiyahudi kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.