Wakalvini


Wakalvini ni Wakristo Waprotestanti wanaofuata kimsingi mafundisho yaliyotolewa awali na Uldrik Zwingli na hasa John Calvin katika karne ya 16.

Ukuta wa Matengenezo mjini Geneva, Uswisi, unawaonyesha wanne kati ya Wakalvini wa kwanza; kutoka kushoto kwenda kulia ni: William Farel, John Calvin, Theodore Beza, na John Knox.

Tofauti na Luther, Zwingli na Calvin walijaribu moja kwa moja kujenga kanisa jipya kwenye msingi wa Biblia.

Hawakupenda kuchukua urithi wowote wa Kanisa Katoliki, wakaunda kila kitu upya kufuatana na jinsi walivyoelewa Biblia.

Katika utawala walikataa cheo cha uaskofu wakaona kanisa liongozwe na wazee wa kuchaguliwa. Kutokana na neno wazee katika lugha ya Agano Jipya (Kigiriki) "presbyuteroi", kanisa lake linaitwa pia la "Wapresbiteri".

Wafuasi wao huitwa pia "Wareformati" (to reform = kutengeneza upya). Maana yake walikataa desturi zote wasizoziona katika Biblia, wakati Luther alizikubali zile alizoziona hazipingi Biblia.

Katika ibada zao, Wareformati wanakataa altari, picha za kupamba kanisa au kuimba liturujia, wakati ibada ya Kilutheri ni Misa ya Kikatoliki iliyobadilishwa kufuatana na mawazo ya Luther. Katika jambo hilo hawakupatana na ndiyo sababu kwa muda mrefu Walutheri na Wareformati walishindwa kuwa na ibada za pamoja, lakini siku hizi wanaelewana.

Mafundisho hayo kutoka Uswisi yalienea katika nchi kama Ufaransa, Uskoti na Uholanzi. Hata Wamoravia walichukua sehemu ya mafundisho ya Wareformati, hasa juu ya Chakula cha Bwana, wakimfuata Luther katika mambo mengine.

Afrika Kusini urithi wa kidini wa Makaburu ni wa Kireformati kwa sababu babu zao walitokea Uholanzi na Ufaransa.

Vilevile ni wamisionari kutoka Uswisi na Uskoti walioanzisha mapema makanisa ya Kipresbiteri Malawi, Kenya na Afrika Magharibi.

Kadiri ya asili, madhehebu yao yanaitwa kwa Kiingereza Reformed, Congregationalists au Presbyterians.

Leo yana jumla ya waamini zaidi ya milioni 80, wengi wao wakiwa wameunganika katika "World Communion of Reformed Churches".

Tanbihi

Marejeo

Marejeo mengine

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wakalvini kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.