Jan Oort

Jan Hendrik Oort (28 Aprili 1900 - 5 Novemba 1992 [1]) alikuwa mwanaastronomia kutoka nchini Uholanzi aliyeweka misingi muhimu ya kuelewa galaksi yetu.

Jan Hendrik Oort (1900 - 1992).

Alitajwa kuwa mmoja wa wanaastronomia muhimu zaidi wa karne ya 20[2] [3]. Wingu la Oort, kwenye sehemu za nje za mfumo wa Jua, lilipewa jina lake.

Maisha

Oort alisoma kwenye Chuo Kikuu cha Groningen. Tangu mwaka 1924 alifanya kazi kwenye paoneaanga mjini Leiden. Tangu mwaka 1945 hadi 1970 alikuwa profesa kwenye Chuo Kikuu cha Leiden pamoja na kuwa mkurugenzi wa paoneaanga.

Utafiti

Anakumbukwa kwa utafiti wake kuhusu tabia za Njia Nyeupe ambamo aliweza kuthibitisha ya kwamba galaksi yetu inazunguka kwenye mhimili wake.

Alionyesha kitovu cha Njia Nyeupe kina umbali wa takriban miakanuru 30,000 kutoka Dunia akakadiria ya kwamba masi ya Njia Nyeupe inalingana na masi ya Jua mara bilioni 100.[4].

Alikuwa pia kati ya wataalamu wa kwanza waliotumia wimbiredio kwa kupima nyota.[5]

Oort alikadiria kuwepo kwa wingu la magimba madogo yanayozunguka mfumo wa Jua letu kwa umbali mkubwa sana ambalo ni asili ya nyotamkia zenye obiti ndefu[6]. Masi hii inaitwa Wingu la Oort. Halikuweza kuthibitishwa bado lakini linalingana na makadirio yote kuhusu mwendo wa nyotamkia.

Kuanzia mwaka 1958 hadi 1961 Oort alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (UKIA).

Marejeo

Viungo vya nje