Waarabu

Waarabu (kwa Kiarabu عَرَبِ, matamshi ya Kiarabu: [ʕarabi]) ni watu ambao lugha mama yao ni Kiarabu wakijitambua vile.

Waarabu duniani
     Jumuiya ya Kiarabu      + 5,000,000      + 1,000,000      + 100,000

Asili ya Waarabu na uenezaji

Kiasili walikuwa watu wa Bara Arabu na maeneo jirani katika Syria na Iraki[1], lakini tangu kuja kwa Uislamu walienea nje ya eneo asilia hasa katika Afrika ya Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati ambako walijichangaya na wenyeji ambao wengi wao wamepokea lugha ya Kiarabu tangu karne nyingi na kujitazama kama Waarabu pia.

Kutokana na uhamiaji wako pia katika Afrika ya Mashariki, Visiwa vya Komoro na visiwa vingine vya Bahari Hindi, Amerika, Ulaya Magharibi, Indonesia, Uhindi na Iran. [2] [3] [4] [5] [6]

Dini ya Uislamu ilianzia kati ya Waarabu na hivyo Kiarabu ndiyo lugha ya Qurani na maandiko ya Kiislamu, na Waarabu wengi ni Waislamu. Walakini kati ya Waislamu wote Waarabu ni kama asilimia 20 tu. [7]

Historia

Kihistoria Waarabu walitajwa mara ya kwanza wakati wa karne ya 9 KK kama makabila ya mashariki na kusini mwa Syria na kaskazini mwa Bara Arabu. [8] Waarabu wanaonekana walikuwa chini ya wafalme wa Milki ya Ashuru (911-612 KK), na baadaye chini ya Milki ya Babeli iliyofuata (626-539 KK), Waakhemi (539-332 KK), Waseleukidi na Waparthi.

Katika karne ya 3 KK Waarabu wa Nabatea waliunda ufalme wao karibu na Petra katika Yordani ya leo. Makabila ya Kiarabu kama Waghassanidi na Walakhmidi huanza kuonekana katika jangwa la Syria Kusini kuanzia katikati ya karne ya 3 BK wakiunda milki zao zilizoshirikiana na Dola la Roma na Wasasani. Hadi karne ya 7 sehemu ya Waarabu hasa wa magharibi mwa eneo lao walikuwa Wakristo, wengine pia Wayahudi.

Baada ya Muhamad, makhalifa wa kwanza (632-661 BK) waliunganisha Waarabu wote chini ya utawala wao wakaendelea kuvamia milki jirani za Dola la Roma na Uajemi ya Wasasani. ote walianza kutumia lugha ya Kiarabu kama lugha ya utawala. Makabila mengi kutoka Bara Arabu yalianza kuhamia nchi zilizovamiwa katika hiyo milki kubwa ya Kiislamu iliyoenea kutoka Moroko na Hispania upande wa magharibi hadi mipaka ya China na Uhindi upande wa mashariki.[9] Katika karne zilofuata, wakazi wengi wa maeneo hayo walianza kuwa Waislamu na kutumia Kiarabu kama lugha ya kidini na ya kielimu; hasa katika sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini pamoja na Misri na katika nchi za Asia Magharibi (hasa nchi za leo Syria, Lebanoni, Iraki) wenyeji wengi walianza kutumia Kiarabu kama lugha yao na hivyo kuitwa Waarabu.

Kwa karne nyingi Waarabu hao walitawaliwa na Milki ya Osmani[10]. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-1918) milki hiyo ilivunjwa na kugawiwa kwa maeneo ya nchi za Kiarabu za leo[11] ambazo kwa muda mfupi zilitawaliwa bado kama makoloni au nchi lindwa chini ya Uingereza na Ufaransa.

Mwaka 1945 nchi hizo ziliunda Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.[12]

Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Nchi za Waarabu

Leo hii Waarabu kimsingi hukalia nchi 22 wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Nchi hizo zinaenea kwa kilomita za mraba milioni 13 kutoka bahari ya Atlantiki upande wa magharibi hadi Bahari ya Kiarabu katika mashariki na kutoka Bahari ya Mediterranean katika kaskazini hadi Pembe ya Afrika na Bahari ya Hindi katika kusini. Watu wasio Waarabu wakitumia lugha zao za pekee huishi pia katika nchi hizo, wakati mwingine wakiwa wengi. Hawa ni pamoja na Wasomali, Wakurdi, Waberberi, Waafar, Wanubi na wengineo .

Uenezaji wa lugha

Wakati wa kuzaliwa kwa Mtume Muhamad lugha ya Kiarabu ilitumika Uarabuni tu, nchi ya jangwa na oasisi. Kutoka hapa makabila ya Waarabu Waislamu walivamia nchi jirani ambako wenyeji walitumia lugha mbalimbali. Lugha kadhaa zimeendelea kwa viwango vidogo, vingine vimebaki na nguvu zaidi. Lugha ya Kiaramu iliyowahi kutamalaki katika siasa na uchumi kuanzia Syria hadi Uajemi na zaidi, imebaki kati watu wa vijiji katika maeneo ya kaskazini ya Syria na Iraki, pia kama lugha ya liturgia kanisani. Kikopti iliyokuwa lugha ya Misri imebaki pekee katika liturgia ya kanisa ilhali Wakristo Wakopti wanaongea Kiarabu tu. Kiberber bado inazungumzwa na milioni kadhaa katika Moroko na Algeria. Kikurdi ina nguvu katika milima ya Syria na Iraki kaskazini. Kiajemi (lugha ya Iran) kimefaulu kurudi kama lugha ya kitaifa lakini imepokea karibu asilimia 40 za msamiati wake kutoka Kiarabu; atahri kubwa ya lugha ya Kiarabu inaonekana pia katika lugha nyingine nyingi hadi Kiswahili.

Katika nchi zinazoitwa Kiarabu, lugha ya Kiarabu imekuwa lugha ya kila siku ya kuongea na pia ya serikali, biashara na utamaduni hata kwa hao ambao bado wmetunza lugha nyingine kama lugha yao ya kwanza[13].

Dini

Kwa upande wa dini, Waarabu huwa na tofauti kati yao.

Katika zama za kabla ya Uislamu, Waarabu wengi walifuata dini za kuabudu miungu mingi. Makabila kadhaa yalikuwa yamekubali Ukristo au Uyahudi na watu wachache waliotwa hanif walisemekana kuwa na imani kwa Mungu mmoja. [14]

Leo, karibu asilimia 93 za Waarabu ni wafuasi wa Uislamu [15]. Kuna pia Wakristo kama jumuiya ndogo zaidi. [16] Waislamu Waarabu kimsingi ni wa madhehebu ya Wasunni, Washiia, Waibadi na Waalawi.

Wakristo wa Kiarabu kwa ujumla hufuata moja ya Makanisa ya Kikristo ya Mashariki, kama yale yaliyo ndani ya makanisa ya Orthodox ya Mashariki, makanisa Katoliki ya Mashariki, au makanisa ya Kiprotestanti ya Mashariki. [17] Kuna pia idadi ndogo ya Wayahudi wa Kiarabu ambao bado wanaishi katika nchi za Kiarabu lakini wengi wao waliondoka kwao wakihamia Israeli au nchi nyingine za Ulaya na Amerika. Sehemu ya Wakristo katika nchi za Kiarabu hawajitambui kuwa Waarabu kwa mfano Wakopti au Waashuri.

Marejeo