Mizani (kundinyota)

Mizani ni kundinyota la zodiaki inayojulikana pia kwa jina lake la kimagharibi la Libra[1]. Ni moja ya makundinyota yanayotambuliwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2]

Nyota za kundinyota Mizani (Libra) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Mizani - Libra jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini
Mizani jinsi ilvyowazwa na msanii Hall

Nyota za Mizani huwa haziko pamoja kihalisi lakini zinaonekana tu vile kutoka duniani. Kwa uhalisi kuna umbali mkubwa kati yao, kama ziko mbali au jirani nasi. Kwa hiyo kundinyota "Mizani" linaonyesha eneo la angani jinsi tunavyoiona kutoka Duniani.

Jina

Mizani ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku. Neno Mizano linatokana na Kiarabu ميزان miizaan ambalo linamaanisha "mizani". Jina hili lilipokelewa na Waarabu kutoka kwa Waroma wa Kale waliosema Libra ("mizani"). Kati ya mataifa ya kale mara nyingi nyota za Mizani zilihesabiwa kuwa sehemu ya Akarabu (nge), pamoja na kuangaliwa kama kundi la pekee.[3] Ptolemaio alitumia jina la Χηλαι khelai inayomaanisha "magando" yaani magando ya nge lakini aliiorodhesha kama kundinyota la pekee[4]. Hii ni pia sababu ya kwamba nyota mbili abngavu zaidi bado zinaitwa "Zubani" yaani magando ya nge.

Mahali pake

Mizani lipo angani kwenye mstari wa Zodiaki kati ya Nadhifa (Virgo) upande wa magharibi na Akarabu (Scorpio) upande wa mashariki.

Magimba ya angani

Mizani huwa na nyota 83 zinazoonekana kwa macho matupu zikiwa na mwangaza unaoonekana wa zaidi ya 6.5 mag. [5]

Nyota angavu zaidi ni Zubani Shimali[6] (Beta Librae au Zubeneschemali) [7]. Ina mwangaza unaoonekana wa mag 2.61 ikiwa na umbali wake unakadiriwa kuwa miakanuru 120 kutoka Dunia[8][9]. Inafuatwa kwa mwangaza na Zubani Junubi. Majina haya yanamaanisha "Koleo ya Kaskazini na ya Kusini", kwa sababu nyota hizi mbili zilitazamiwa zamani pia kuwa sehemu ya kundinyota jirani ya Saratani, ambako yalimaanisha koleo za "saratani" au kaa.

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miakanuru)
Aina ya spektra
β27Zubeneschemali (Zubani Shimali)2,61m120B8 V
α29Zubenelgenubi (Zubani Junubi)2,75m77A3
σ203,29m292M3 III
υ3,60m
θ393,6m120K4 III
τ403,66m400B3 V
γ383,91m152G8 IV
Habari za mwangaza na umbali vinaweza kubadilika kutokana na vipimo vipya

Tanbihi

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 269 ff (online kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Toomer, G.J. : Ptolemy's Almagest, translated and annotated by G.J. Toomer, London 1984, ISBN 0-7156-1588-2 online hapa


Makundinyota ya Zodiaki
Majina ya kisasa yanafuatwa kwa mabano na jina la mabaharia na jina la Kilatini (la kimataifa)

Kaa (Saratani – Cancer )Kondoo (Hamali – Aries )Mapacha (Jauza – Gemini )Mashuke (Nadhifa – Virgo )Mbuzi (Jadi – Capricornus )MizaniLibra ) • Mshale (Kausi – Sagittarius )Ndoo (Dalu – Aquarius )Nge (Akarabu – Scorpius )Ng'ombe (Tauri – Taurus )Samaki (Hutu – Pisces )Simba (Asadi – Leo )