Boko Haram

Boko Haram ni kundi la Waislamu wenye itikadi kali kaskazini mwa Nigeria; lina mwelekeo wa kijihadi na kutumia mbinu za ugaidi. Kutoka Nigeria wameingia pia katika nchi jirani za Chadi, Niger na Kamerun ya Kaskazini[1].

Majeruhi wa mashambulizi ya Boko Haramu

Jina

Jina "Boko Haram" linatokana na lugha ya Kihausa likimaanisha "vitabu ni haramu" yaani "elimu ya kimagharibi ni haramu au dhambi".

Historia

Boko Haram ilianzishwa na Yusuf Mohamed mwaka 2002 na inalenga kuanzisha dola la Kiislamu katika nchi Nigeria ambako sharia ni sheria ya pekee.[2][3]

Tangu mwaka 2010 kundi hilo linatumia jina rasmi la ‏جماعة أهل السنة للدعوة والجهاد‎, jamāʿat ahl as-sunna li-d-daʿwa wa-l-ǧihād, yaani "jumuiya ya watu wa Sunna kwa ajili ya uenezaji (wa Uislamu) na jihadi".[4]

Imekadiriwa ya kwamba mapigano yaliyoanzishwa na Boko Haram au kutekelezwa dhidi yake yamesababisha vifo vingi, Rais wa Nigeria Jonathan Goodluck alidai Mei 2014 kuwa kundi lilisababisha vifo vya watu 12,000 na wajeruhiwa kwa maisha 8,000. [5][6][7][8][9][10][11]

Baada ya kushambulia shule, vituo vya polisi,makanisa na ofisi za serikali kundi lilitoa tamko mwaka 2012 kuwa linawapa Wakristo wote nafasi ya siku 3 kuondoka kaskazini mwa Nigeria au watauawa. Tangu tangazo lile mashambulio yameongezeka. Hawashambulii Wakristo na mapolisi pekee lakini pia idadi kubwa ya Waislamu ambao ndio wakazi wengi kaskazini.

Mnamo Aprili 2014 kundi la Boko Haram likashambulia mji wa Chibok katika jimbo la Borno, likaweka moto na kuharibu nyumba 170 na kuingia shule ya sekondari walipokamata wasichana zaidi ya 200, Tarehe 6 Mei 2014, wasichana wengine 8 walitekwa na watu wenye silaha wanaofikiriwa kuwa wa kundi hilohilo.[12][13] Kiongozi wa Boko Haram, Shekau alitisha kuwauza mabinti kama watumwa[14].

Tarehe 12 Mei 2014 video ya Boko Haram ilidai kuwa mabinti wote waweongokea Uislamu na watashikwa hadi wafungwa wa Boko Haram waliomo mkononi mwa serikali watakapoachishwa na kuwekwa huru. .[15]

Tanbihi