Chama cha Kijani cha Ujerumani

Chama cha Kijani cha Ujerumani (Kiing. Green Party, jina rasmi la Kijerumani Bündnis 90/Die Grünen) ni chama cha kisiasa nchini Ujerumani. Mara nyingi huitwa tu "Wakijani" (Kiing. The Greens, Kijer. Die Grünen).

Nembo ya Chama cha Kijani cha Ujerumani

Kilianzishwa mwaka 1992 kwa maungano ya chama cha Ujerumani Magharibi Die Grünen na chama cha Ujerumani Mashariki Bündnis '90. Chama kinakazia hifadhi ya mazingira na ekolojia, haki za kiraia, usawa kati ya wanaume na wanawake na nafasi za wahamiaji katika jamii ya Ujerumani.

Historia

Katika miaka ya 1970, kulikuwa na maandamano mengi dhidi ya upanuzi wa nishati ya nyuklia nchini Ujerumani. Waandamanaji hawakuwa na uungwaji mkono katika vyama vya siasa nchini Ujerumani hivyo wakapata wazo la kuunda chama chao[1].

Chama hicho kilianzishwa kwa jina la "Die Grünen" ("Wakijani", kwa maana ya wanaekolojia) huko Karlsruhe tarehe 13 Januari 1980.

Harakati hizo kwa haki za kiraia na ekolojia ziliungana na mwendo dhidi ya kuongezeka kwa silaha za nyuklia wakati wa vita baridi baina ya nchi za NATO na nchi za kikomunisti (Mapatano ya Warshawa). Greens walikuwa wapinzanivita wakapinga silaha za nyuklia. Walitaka kufikia Ulaya isiyo na jeshi. Baada ya muda mfupi baadhi ya watu wa mrengo wa kulia walihama chama, hivyo wakawa chama cha mrengo wa kati. Chama kina mirengo ya kati na kushoto.

Mnamo mwaka 1983 Wakijani walifaulu mara ya kwanza kupata asilimia 5 za kura katika uchaguzi mkuu wakaingia katika Bundestag wakarudishwa mwaka 1987 kwa 8,3%. Lakini baada ya muungano wa Kijerumani mwaka 1990 walishindwa kurudi bungeni.

Wakijani katika mashariki ya Ujerumani

Mnamo 1990, wakati wa mwisho wa ukomunisti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani, vyama vipya viliundwa katika mashariki ya Ujerumani pamoja na Chama cha Kibichi na vyama vya kupigania haki za kiraia. Kwa ajili ya uchaguzi wa kwanza baada ya maungano ya Ujerumani viliungana pamoja kwa jina la "Bündnis 90" yaani "Maungano ya 1990".

Ilhali Chama cha kibichi cha magharibi ilishindwa kupata asilima 5 za kura na hivyo hakikuingia katika bunge, maungano ya mashariki yalipita 8% na kuingia bungeni.

Maungano ya vyama na kuingia serikalini

Mara baada ya uchaguzi, vyama vya Kibichi vya mashariki na magharibi viliungana[2].

Mwaka 1994 chama kiliweza kurudi bungeni ambako kimeendelea kuwa na kundi la wabunge.

Mwaka 1998 kiliingia katika serikali ya ushirikiano na chama cha SPD chini ya chansela Gerhard Schröder. Wakijani walipata mawaziri watatu. Katika kipindi hicho waliona changamoto kutokana na vita ya Kosovo iliyotokea baada ya kuporomoka kwa Yugoslavia. Mawaziri wao walitaka jeshi la Ujerumani lijiunge na vikosi vya NATO vilivyotetea Kosovo dhidi ya Serbia ambayo ilikuwa kinyume cha upinzani-vita. Wanachama walianza kutoka kwenye chama, na kura zilipungua kwenye chaguzi za vieneo.

Lakini makubaliano ya kuondoka kwa Ujerumani katika nishati ya kinyuklia pamoja na kukataa kwa serikali ya kujiunga na Vita ya pili ya Ghuba dhidi ya Iraki yaliimarisha chama tena. Serikali haikuweza kuendelea baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 kwa sababu ya kushuka kwa kura za SPD.

Upinzani kitaifa na serikali kijimbo

Katika miaka iliyofuata Chama cha kijani kiliendelea kuwa upande wa upinzani katika bunge la shirikisho lakini kilingia katika serikali mbalimbali kwenye ngazi ya majimbo[3].

Mwaka 2011 kilifaulu kuwa chama kikubwa zaidi katika bunge la Baden-Württemberg na kushika nafasi ya waziri mkuu anayeongoza serikali ya jimbo katika ushirikiano na chama kidogo zaidi[4].

Serikalini tangu 2021

Mwaka 2021 chama kilifaulu pia katika uchaguzi mkuu na kuwa chama cha tatu kwenye Bundestag. Kikaingia katika serikali ya ushirikiano na SPD chini ya chansella Olaf Scholz na pamoja na chama cha liberali FDP[5].

Matokeo ya uchaguzi

Yafuatayo ni matokeo ya Wakijani kwenye uchaguzi wa Bundestag, bunge la kitaifa.

Uchaguzi mkuuKura kwenye majimbo ya uchaguziKura za chama kitaifaWabunge
(Kijani/wabunge wote)
+/–Nafasi
Kura%Kura%
1980732,6191.0 (#5)569,5891.5 (#5)0/497(nje ya bunge)
19831,609,8554.1 (#5)2,167,4315.6 (#5)27/498 27Upinzani
19872,649,4597.0 (#4)3,126,2568.3 (#5)42/497 15Upinzani
1990[6]2,589,9125.6 (#5)2,347,4075.0 (#4)8/662 36Upinzani
19943,037,9026.5 (#4)3,424,3157.3 (#4)49/672 41Upinzani
19982,448,1625.0 (#4)3,301,6246.7 (#4)47/669 2Serikalini na SPD
20022,693,7945.6 (#5)4,108,3148.6 (#4)55/603 8Serikalini na SPD
20052,538,9135.4 (#5)3,838,3268.1 (#5)51/614 4Upinzani
20093,974,8039.2 (#5)4,641,19710.7 (#5)68/622 17Upinzani
20133,177,2697.3 (#5)3,690,3148.4 (#4)63/630 5Upinzani
20173,717,4368.0 (#6)4,157,5648.9 (#6)67/709 4Upinzani
20216,465,50214.0 (#3)6,848,21514.8 (#3)118/735 51Serikalini na SPD na FDP

Marejeo

Viungo vya Nje