Mlipuko wa homa ya mafua wa 1918

Mlipuko wa homa ya mafua wa 1918 (unaojulikana pia kama Spanish Flu) ulikuwa pandemia ya homa ya mafua iliyotokea kwenye mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Ulidumu miaka mitatu, kuanzia Januari 1918 hadi Desemba 1920. [1] Takriban watu milioni 500[2] waliambukizwa duniani kote ilhali wakati ule idadi ya watu duniani ilikuwa milioni 1,800 tu.

Wodi ya wagonjwa wa Homa ya Mafua kwenye hospitali ya dharura ya kijeshi, huko Camp Finston, Kansas, Marekani.
Idadi ya vifo vya pandemia huko New York, London, Paris na Berlin.

Ugonjwa uliosambaa shauri ya Vita Kuu

Usambazaji wake uliathiriwa na vita ambako wanajeshi na wafanyakazi walisafirishwa kwa idadi kubwa kati ya mabara yote, pia kutokana na njaa iliyosambaa katika sehemu nyingi za dunia wakati wa vita na kudhoofisha watu wengi.

Pandemia hiyo iliua baina ya watu milioni 50 hadi 100[3] - waliokuwa sawa na asilimia 3 hadi 5 ya watu wote duniani wakati huo. [3] Hii inamaanisha kuwa lilikuwa moja ya maafa asilia mabaya zaidi katika historia. [2] [4] [5] [6]

Jina la "Spanish Flu"

Jina "mafua ya Kihispania" (Spanish Flu) lilitokana na taarifa juu ya ugonjwa katika magazeti ya Hispania; hali halisi nchi nyingine za Ulaya ziliathiriwa vibaya zaidi lakini serikali za nchi zilizoshiriki vitani zililenga kuficha habari za vifo vingi [7] [8]; ilhali Hispania haikushiriki vita, hivyo magazeti yalikuwa na uhuru. Kwa hiyo taarifa katika magazeti yake yalileta picha isiyo ya kweli kuwa ugonjwa ulianza Hispania[9].

Tabia za ugonjwa

Virusi vilisambaa duniani kwa mawimbi matatu. Wimbi la kwanza mwanzoni wa mwaka 1918 halikuwa na nguvu sana, na pale lilipopita watu walianza kujenga kinga dhidi ya mawimbi yaliyofuata. Wimbi kuu lilianza kwenye Oktoba/Novemba 1918 na kuua watu wengi. Iliathiri zaidi Afrika ambako wimbi la kwanza halikufika. Wimbi la tatu liliendelea hadi 1920 lakini halikuwa kali vile kwa sababu watu wengi waliwahi kuambukizwa na hivyo kuwa na kinga[10].

Tabia ya pekee ya pandemia hiyo ilikuwa kwamba homa ya mafua kwa kawaida inasababisha vifo kati ya watoto wadogo na wazee, lakini mlipuko huo uliua hasa vijana na watu wazima wenye umri wa wastani.

Hakuna data za kutosha ili kuhakikisha mahali ambapo ugonjwa huo ulipoanzia. [2] Virusi vyake vilikuwa vya aina H1N1. Mabadiliko ya aina hiyo yalirudi katika karne ya 20 na 21 yakisabisha pandemiki mpya.

Athari katika Afrika ya Mashariki

Tanganyika iliona mapigano kwa miaka yote ya Vita Kuu hadi Novemba 1918. Wanajeshi kutoka nchi jirani kama Kenya, Rhodesia (Zambia) na Kongo, kutoka Afrika Kusini, Ulaya na Uhindi waliingia na kurudi na kusambaa virusi vyake, pamoja na wapagazi elfu nyingi waliolazimishwa kubeba mizigo yao. Mapigano yaliwahi kuleta uharibifu na njaa ilhali askari walichukua vyakula vyote walivyokuta katika nchi ambako ukosefu wa barabara ulileta ugumu wa kupeleka vyakula hadi vikosi kwenye pori.

Maambukizi ya kwanza yalitambuliwa Mombasa, Kenya mnamo Septemba 1918[11]. Ugonjwa ulifika kwa meli kutoka Uhindi. Kutoka hapa ulisambaa haraka pamoja na wapagazi wa Carrier Corps walioachishwa na kubeba virusi hadi makwao nyumbani.[12]

Virusi vilienea haraka hadi Tanganyika iliyotawaliwa wakati ule na majeshi wa Uingereza na Ubelgiji, ilhali vikosi vya Wajerumani walipatikana kwenye kanda nyembamba la kusini. Waingereza walipoanza kujenga serikali yao kwenye mwisho wa 1918, walikadiria kuwa nusu ya watu wote aliathiriwa. Katika eneo la Tukuyu lenye wakazi 180,000, takriban asilimia 10 au watu 18,000 walikufa. Makadirio ya vifo vyote katika Tanganyika hutaja vifo 100,000 (eneo lote lilikuwa na wakazi milioni 4 kabla ya vita). Zanzibar pekee iliweza kuthibiti mlipuko kwa sababu serikali ilichukua hara hatua za kutenganisha wagonjwa na kuwafuatilia.[13]

Picha

Marejeo