Mpira wa miguu

mchezo ambayo ni kati ya timu mbili za wachezaji kumi na moja

Mpira wa miguu (pia soka au kandanda) ni mchezo unaochezwa na jumla ya wachezaji ishirini na wawili katika timu mbili, kila timu ikiwa na wachezaji kumi na mmoja.

Mechi ya kandanda ya Angola dhidi ya Moroko mwaka 2013.

Lengo hasa la mchezo huu ni wachezaji kuumiliki mpira kwa kutumia miguu na kufunga goli, yaani kuuingiza mpira katika wavu wa wapinzani mara nyingi zaidi.

Matumizi ya mikono ni marufuku isipokuwa kwa mlinda mlango katika eneo maalumu na wakati wa kurudisha mpira baada ya kutoka nje ya uwanja.

Historia

Mchezaji wa mpira wa miguu, Ugiriki ya Kale.

Michezo mbalimbali ya kuchezea mpira inaweza kupatikana katika kila uwanja wa jiografia na historia. Wachina, Wajapani, Wakorea na Waitalia, wote hao walikuwa wakicheza mpira zamani kabla ya enzi zetu. Wagiriki na Waromania walitumia michezo hiyo kuwaandaa wapiganaji kabla ya vita.

Hata hivyo, ni nchini Uingereza ambapo umbo la soka la kisasa lilianza kulipuka.

Ilianza wakati mashirikisho mawili (Shirikisho la Mpira wa miguu na Mpira wa Ragbi) yalipotawanyika. Shirikisho la kwanza lilibakia Uingereza. Mnamo Oktoba 1963, Vilabu 11 vya London vilituma wawakilishi katika mkutano wa Freemasons ili kujadili na kuweka kanuni zilizokubalika kusimamia mechi zilizochezwa kati yao.

Mkutano huu ulipelekea kuanzisha kwa Shirikisho la Kandanda (Football Association).

Miongoni mwa kanuni zilizowekwa ni zile za kukataa utumiaji wa mikono kushika mpira na kunyang'anyana kwa nguvu. Soka na Ragbi zilifarakana tarehe hiyo.

Miaka minane baada ya kuanzishwa, Shirikisho la Kandanda (FA) lilikuwa na wanachama 50. Shindano la kwanza la kandanda - Kombe la FA - lilianza mwaka huo, likifuatiwa na lile la Ligi ya Ubingwa miaka 17 baadaye.

Wachezaji wawili wa Klabu ya Darwin, John Dove na Fergus Suter walikuwa wa kwanza kulipwa kwa mchezo wao. Kitendo hiki kilikuwa mwanzo wa soka la kulipwa iliyohalalishwa mwaka wa 1885.

Mwamko huu ulipelekea kuanzishwa kwa Mashirikisho ya kitaifa nje ya Uingereza (Great Britain). Baada ya Shirikisho la Kandanda la Uingereza, Mashirikisho yaliyofuatia ni ya Uskoti (1873), Wales (1875) na Eire (1880).

Kutokana na ushawishi mkuu wa Uingereza katika mataifa ya dunia, soka ilisambaa kote duniani.

Mataifa mengine mengi yalianzisha Mashirikisho ya Kandanda kufikia 1904 wakati Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) lilipoanzishwa. Tangu hapo, kandanda ya kimataifa imekuwa ikikua licha ya vikwazo mbalimbali.

Kufikia 1912, FIFA ilikuwa na uanachama wa mashirikisho 21, idadi iliyoongezeka na kufikia 36 mwaka 1925.

Kufikia 1930 - mwaka ambapo kwa mara ya kwanza kulikuwa na mashindano ya Kombe La Dunia, FIFA ilikuwa na wanachama 41. Idadi hii ilizidi kuongezeka na kufika 51 mnamo 1938 na 76 kufikia 1950.

Baada ya Kongamano la FIFA la mwaka 2000, kulikuwa na wanachama 204 na idadi hii inazidi kukua kila mwaka.

Kanuni

Maagizo ya Kandanda hupitiwa na kufanyiwa mabadiliko kila mwaka (Mwezi Julai) na Shirikisho la Kandanda Duniani (FIFA).[1]

Uwanja

Vipimo vya uwanja wa soka.

Uwanja una umbo la mstatili. Hakuna kipimo kamili, ila kanuni zinasema urefu ni baina ya mita 90 na 120, upana baina ya mita 45 na 90. Kwa michezo ya kimataifa urefu uwe baina ya mita 100 - 110 na upana baina ya mita 64 na 75.

Goli ziko kwenye pande fupi zaidi. Kuna alama ya bendera kwenye kona za uwanja. Mwaka 2008 IFAB ilijaribu kusanifisha vipimo kuwa mita 105 kwa 68, lakini kanuni hii ilisimamishwa baadaye.

Mstari ni mpaka wa uwanja. Wakati mpira uko kwenye mstari hata kwa kiasi kidogo unahesabiwa bado uko ndani ya uwanja. Kwa goli kukubaliwa sharti mpira uwe umepita mstari wa goli kabisa.

Mpangilio wa wachezaji

[2][3]Kuna wachezaji wa aina tatu: beki, kiungo na washambuliaji au straika na golikipa .

Ni uamuzi wa kocha kuhusu idadi ya wachezaji wa kulinda lango, wa kiungo au wa mbele, ikitegemea mfumo uliotumika. Mfumo wa 4-4-2[4] umekuwa maarufu miongoni mwa timu nyingi. Mfumo huu hujumlisha walinzi wanne pamoja na mlinda lango, wachezaji wanne wa kiungo na wawili wa mbele.mshambuluaji lazima akawa mtu mwenye ujuzi mkubwa na mwenye nguvu za kushambulia

Utunukizi wa Alama

Golikipa akiokoa mpira uliopigwa shuti ndani ya eneo la penati

Katika ligi za kitaifa na kimataifa, alama hutunukiwa kwa timu baada ya mchezo. Timu iliyoshinda hupewa alama tatu huku timu zilizotoka sare hupewa alama moja kila moja.

Ikiwa ni lazima mshindi apatikane, hasa kwenye mechi za fainali, mchezo huwa na muda wa ziada kama timu hizo ziko sare. Iwapo sare hiyo huendelea mchezo huamuliwa kwa mikwaju ya penalty.

Shirikisho la Kandanda Duniani

[5]Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) ndilo shirikisho kuu linalosimamia kandanda duniani. Wanachama wake ni mashirikisho ya kandanda ya nchi mbalimbali. Kufikia mwaka wa 2000, lilikuwa na wanachama 204 kutoka pembe zote za dunia. Shirikisho hili huandaa mashindano mbalimbali ya soka kama vile Kombe la Dunia la FIFA na pia huwatunuku wachezaji.

Orodha ya Wachezaji Maarufu Duniani

Orodha ifuatayo inaonyesha baadhi ya wanasoka maarufu duniani, lakini haiashirii usanjari huu kulingana na ubora. Wapo wengine wengi ambao hawajatajwa hapa.[6]

Orodha ya wachezaji duniani waliofunga zaidi ya magoli 500

MchezajiMagoliMichezoG/MMiaka
1 Cristiano Ronaldo83811840.712001
2 Lionel Messi82310630.772003
3 Josef Bican8125221.561931-1957
4 Romario7729940.781985-2009
5 Pelé7678120.941956-1977
6 Ferenc Puskas7467540.991943-1966
7 Gerd Muller7357930.931962-1981
8 Abe Lenstra6767770.871936-1963
9 Robert Lewandowski6419130.702005
10 Zlatan Ibrahimovic5799940.581999
11 Ferenc Deak5765101.131940-1957
12 Tulio Maravilha5757940.721988-2019
13 Uwe Seeler5755920.971953-1978
14 Godfrey Chitalu5698110.701964-1982
15 Ernst Willimowski5544741.171934-1955
16 Eusebio5526390.861957-1980
17 Jimmy McGrory5505471.011922-1938
18 Franz Binder5464301.271930-1949
19 Fernando Peyroteo5443541.541937-1950
20 Hugo Sánchez5418950.601976-1998
21 Luis Suárez5408960.602005
22 Fritz Walter5395720.941937-1959
23 Jozsef Takacs5235260.991917-1934
24 Gyula Zsengeller5226410.811935-1953
25 Zico5227880.661971-1994
26 Alfredo Di Stefano5147060.731945-1966
27 Hans Krankl5146550.781970-1989
28 Gunnar Nordahl5135610.911937-1958
29 Roberto Dinamita5128250.621971-1992
30 Jimmy Greaves5118120.631957-1971
31 Ferenc Bene5089460.541961-1979

Mpira wa miguu barani Afrika

Mchezo ulipelekwa Afrika na Waingereza wakati wa ukoloni. Mechi za kwanza zilizorekodiwa mwaka 1862 huko Cape Town na Port Elizabeth[7].

Ilhali ulikuwa mwanzoni mchezo wa kizungu ulienea haraka kati ya vijana Waafrika kupitia shule, jeshi na wafanyakazi wa reli. Kwa mfano kisiwani Unguja walikuwa wafanyakazi Wazungu na Wahindi waliocheza soka pamoja wakitazamiwa na wenyeji, halafu wanafunzi wa shule ya misioni St Andrew's ya UMCA. Khamis Fereji alikumbuka jinsi gani mnamo 1910 soka ilichezewa na watoto na vijana kote Zanzibar mjini wakitumia mipira ya tennis mtaani au mwambanoni wakati wa jioni ilhali wazee walitazama. Vivyi hivyo aliandika Dr. Nmandi Azikiwe katika kumbukumbu ya maisha yake ya kwamba alipokuwa mtoto Calabar (Nigeria) kabla ya Vita Kuu ya Kwanza walicheza mpira kila mahali kwa kutumia maembe, machungwa au mipira ya tennis[8]

Mchezo ukaendelea kupanuka na kuendeshwa na wenyeji katika klabu zilizoundwa wakati miji ilikua na kuwa na wakazi wengi Waafrika[9].

Tangu uhuru soka ilipanuka sana katika nchi huru za Afrika. Baada ya kujiunga na FIFA wawakilishi wa nchi huru za Afrika waliweza kuhakikisha ya kwamba Afrika Kusini ilitengwa kwa sababu ya siasa yake ya apartheid (ubaguzi wa rangi).

Tangu 1970 mpango wa kombe la dunia ulibadilishwa kuhakikisha nafasi kwa kila bara na Afrika ilipewa nafasi 1 ya hakika. 1986 zilikuwa nafasi 2, 1998 nafasi 4 na tangu kombe la 2002 kuna nafasi 5 kwa timu kutoka Afrika. [10]

Kwa Tanzania na nchi nyingi za Afrika kuna uhaba wa wafadhiliː hiyo husababisha timu ambazo hazina uwezo wa kiuchumi kukata tamaa. Tatizo kubwa ni uhamisho wa wachezaji vijana wenye uwezo kuhamia nje ya Afrika. Wakati wa kombe la dunia idadi kubwa wachezaji wa timu za kitaifa kutoka Afrika wanaajiriwa na klabu huko Ulaya; wakati wa kombe la dunia dunia 2010 walikuwa asilimia 80 za wachezaji Waafrika kwenye kombe la dunia waliocheza kwa klabu za Ulaya. Hali hii inashusha uwiano wa soka katika ligi za kitaifa kwa sababu wachezaji bora wako ng'ambo wakipatikana tu kwa mechi za kimataifa wakishiriki katika timu ya kitaifa.[11]

Mpira wa miguu nje ya kanuni za kawaida

Video inaonyesha namna nyingi jinsi gani mpira unachezewa duniani.
Katika mpira wa miguu, madhumuni ya msingi ya mashabiki ni kuhamasisha timu yao wakati wa mechi.

Hali halisi kuna namna nyingi kucheza soka hata pasipo na wachezaji 22 au uwanja kamili. Kila mahali dunaini watu hasa vijana hucheza barabarani au shambani kwa kila idadi ya wachezaji, ilhali fimbo au mawe mawili hudokeza goli. Pasipo na mpira kamili vijana hujitengenezea kifaa kwa karatasi au plastiki iliyoshikwa kwa kamba katika umbo la kufanana na tufe.

Kwa mazingira ya pekee kuna pia mapatano juu ya kanuni maalumu kwa timu ndogo (kwa mfano wachezaji 5/5) au mahali kama mchanga wa mwabaoni (beach soccer), katika ukumbi (indoor soccer) au kwa wachezaji walemavu.

Tanbihi

Tazama pia

Viungo vya nje