Italia

nchi katika Ulaya Kusini

Jamhuri ya Italia (kwa Kiitalia: Repubblica Italiana) ni nchi ya Ulaya Kusini inayoenea katika sehemu kubwa ya Rasi ya Italia na baadhi ya visiwa vya jirani kwenye Bahari ya Kati.

Repubblica Italiana
Jamhuri ya Italia
Bendera ya ItaliaNembo ya Italia
Lugha rasmiKiitalia; kijimbo pia Kijerumani, Kifaransa, Kiladino, Kislovenia, Kisardinia
Mji MkuuRoma
RaisSergio Mattarella
Waziri MkuuMario Draghi
Eneokm² 302,072.84
Wakazi59,236,213 (31-12-2020) (23º duniani)
Wakazi kwa km²201.7
JPT31,022 US-$ (2008)
PesaEuro
WakatiUTC+1
Wimbo wa TaifaFratelli d'Italia (Ndugu wa Italia)
Sikukuu ya Jamhuri2 Juni
Sikukuu ya Ukombozi25 Aprili
Simu ya kimataifa+39
Italia katika Ulaya na katikati ya Bahari ya Kati.
Ramani ya Italia
Italia jinsi inavyoonekana kutoka angani

Eneo lake ni km² 302,072.84 ambalo lina wakazi 59,236,213 (31-12-2020): ni nchi ya 23 duniani kwa wingi wa watu, lakini ya 8 au 9 kwa uchumi. Mtu anayetokea katika nchi hii ya Italia kwa Kiswahili huitwa Mwitalia.

Imepakana na Ufaransa, Uswisi, Austria na Slovenia. Nchi huru mbili ndogo zinazozungukwa na eneo la Italia pande zote ni San Marino na Vatikano.

Makao makuu ni jiji la Roma, lenye umuhimu mkubwa katika historia ya dunia nzima.

Jiografia

Umbo la jamhuri, kama lile la rasi yake, linafanana na mguu linalozungukwa na maji ya Mediteraneo pande tatu.

Milima ya Appennini inaunda uti wa mgongo wake, wakati ile ya Alpi, ambayo ni mirefu zaidi, inaunda kwa kiasi kikubwa mpaka kati ya Italia na nchi nyingine za Ulaya.

Mlima mrefu zaidi, ukiwa na mita 4,810 juu ya usawa wa bahari, unaitwa Monte Bianco (Mlima Mweupe) na uko mpakani kwa Ufaransa.

Visiwa viwili vikubwa vya Sisilia na Sardinia ni sehemu za Italia pamoja na visiwa vingi vidogovidogo, vile vya Pelagie vikiwa upande wa Afrika.

Italia ina volkeno 14, ambazo 4 kati yake ziko hai: ile ndefu zaidi kuliko zote za Ulaya (mita 3,329) inaitwa Etna na iko mashariki mwa Sisilia. Italia inaongoza Ulaya kwa wingi wa matetemeko ya ardhi.

Mto mrefu zaidi unaitwa Po na una urefu wa kilomita 652. Mito mingine mirefu ni Adige, Tevere, Adda, Oglio, Tanaro, Ticino, Arno, Piave, Reno, Sarca-Mincio n.k.

Maziwa makubwa zaidi ni: Garda (km2 367.94), Ziwa Maggiore (212.51, likiingia Uswisi), Ziwa la Como (145.9), Trasimeno (124.29) na Ziwa la Bolsena (113.55).

Kutokana na urefu mkubwa wa Italia toka kaskazini hadi kusini, hali ya hewa ni tofauti sana, kuanzia baridi kali sana hadi joto kali sana.

Mikoa

BenderaJinaMakao makuuEneo (km2)WakaziMsongamano wa watu/km²WilayaMijiMiji mikubwaHali ya utawala
AbruzzoL'Aquila10,7631,307,9191224305-Kawaida
Bonde la AostaAosta3,263126,93339074-Kujitawala
PugliaBari19,3584,045,9492096258BariKawaida
BasilicataPotenza9,995575,902582131-Kawaida
CalabriaCatanzaro15,0811,954,4031305409Reggio CalabriaKawaida
CampaniaNapoli13,5905,761,1554245551NapoliKawaida
Emilia-RomagnaBologna22,4464,354,4501949348BolognaKawaida
Friuli-Venezia GiuliaTrieste7,8581,219,3561554218TriesteKujitawala
LazioRome17,2365,550,4593225378RomeKawaida
LiguriaGenoa5,4221,565,3492894235GenoaKawaida
LombardiaMilan23,8619,749,593409121544MilanKawaida
MarcheAncona9,3661,541,6921655239-Kawaida
MoliseCampobasso4,438312,394702136-Kawaida
PiemonteTurin25,4024,366,25117281206TurinKawaida
SardiniaCagliari24,0901,637,193688377CagliariKujitawala
SisiliaPalermo25,7114,994,8171949390Catania, Messina, PalermoKujitawala
Trentino-Alto Adige/SüdtirolTrento13,6071,036,707762333-Kujitawala
ToscanaFirenze22,9943,679,02716010287FirenzeKawaida
UmbriaPerugia8,456885,535105292-Kawaida
VenetoVenisi18,3994,865,3802647581VenisiKawaida

Historia

Makala kuu: Historia ya Italia
Mji wa Venisi, uliojengwa juu ya visiwa 117.
Mnara wa Pisa, pamoja na kanisa kuu la Pisa na batizio yake.
Ikulu ya Caserta.

Akiolojia imethibitisha uwepo wa Homo neanderthaliensis miaka 128,000-187,000 hivi iliyopita. Homo sapiens sapiens alifika miaka 40,000 hivi iliyopita.

Kufikia milenia ya 1 KK wakazi wengi walikuwa wa jamii ya Kizungu na kutumia lugha za Kihindi-Kiulaya.

Peninsula ya Italia iliunganishwa mara ya kwanza na Jamhuri ya Roma (509-27 KK), lakini hiyo ilipoenea Ulaya kusini na magharibi, Afrika ya Kaskazini na Asia ya Magharibi ikawa na sura ya kimataifa kama Dola la Roma.

Umoja ulipotea kuanzia uvamizi wa jiji la Roma uliofanywa na Wagermanik (476 BK) na hasa baada ya ufalme wa Karolo Mkuu aliyetawala sehemu ya kaskazini tu.

Juhudi za kuurudisha umoja zilifanywa hasa katika karne ya 19, ambapo Ufalme wa Sardinia uliteka sehemu kubwa ya Italia (hasa miaka 1860, 1866 na 1870) na kubadilika kuwa Ufalme wa Italia wenye makao makuu Roma.

Baada ya vita vikuu vya pili iligeuka Jamhuri yenye katiba inayotia mamlaka kuu mikononi mwa bunge.

Ni kati ya nchi sita zilizoanzisha Umoja wa Ulaya mwaka 1957 ikaendelea kuunga mkono ustawi wake hadi uanzishaji wa pesa ya pamoja (Euro).

Maendeleo

Italia ni kati ya nchi zilizoendelea, ikiwa na nafasi ya nane kwa nguvu ya uchumi duniani, hivyo ni mwanachama wa G7, G8 na G20.

Sanaa na utalii

Kuanzia kushoto kwa kufuata mzunguko wa mishale katika saa: Kanisa kuu la Florence, lenye kuba la matofali kubwa kuliko yote duniani;[1][2] Basilika la Mt. Petro, kanisa kubwa kuliko yote duniani, liko Vatikani, nchi inayozungukwa na Italia pande zote;[3] kanisa kuu la Milano, la tano duniani kwa ukubwa;[4] na Basilika la Mt. Marko, Venezia.[5]

Italia ndiyo nchi inayongoza duniani kwa kuwa na mahali pengi (51) pa kimaumbile na pa kihistoria palipoingizwa katika orodha ya UNESCO ya "Urithi wa Dunia".

Kwa sababu hiyo pia inashika nafasi ya 5 kati ya nchi zote zilizo lengo la utalii.

Watu

Wananchi wana sifa za pekee kati ya Wazungu wote, hata upande wa DNA, kutokana na jiografia na historia ya rasi.

Ni kati ya nchi ambamo watu wanatarajiwa kuishi miaka mingi zaidi, lakini pia ni kati ya nchi ambapo uzazi ni mdogo zaidi: wanaokufa ni wengi kuliko wanaozaliwa.

Kutokana na umati wa Waitalia waliohama nchi hiyo karne za nyuma, sasa zaidi ya watu milioni 60 nje ya Italia wana asili ya nchi hiyo, mbali na raia zaidi ya milioni 4 wanaoishi nje.

Lugha rasmi ni Kiitalia, inayotegemea zaidi lahaja za Italia ya Kati, lakini siku hizi inatumiwa na wananchi walio wengi hata katika mikoa mingine, ambayo kwa jumla ni 20.

Upande wa dini, wengi wao (81.2%) ni Wakristo wa Kanisa Katoliki, wakifuatwa na Waorthodoksi (2.8%, wengi wao wakiwa wahamiaji, hasa kutoka Romania) na Waprotestanti (1.1%, wengi wao wakiwa Wapentekoste). Uhamiaji mwingi wa miaka ya mwisho wa karne ya 20 umeleta pia Uislamu (3.7%) na dini nyingine.

Dini zote zinaachiwa uhuru na, tofauti na nchi nyingi za Ulaya, waumini wake wanajitahidi kiasi kufuata ibada (29% kila wiki).

Watu maarufu

Tazama pia

Tanbihi

Marejeo

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Nchi za Umoja wa Ulaya
Austria | Bulgaria | Eire | Estonia | Hispania | Hungaria | Italia | Kroatia | Kupro | Latvia | Lituanya | Luxemburg | Malta | Polandi | Slovakia | Slovenia | Romania | Ubelgiji | Ucheki | Udeni | Ufaransa | Ufini | Ugiriki | Uholanzi | Ujerumani | Ureno | Uswidi
Makala hii kuhusu maeneo ya Italia bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Italia kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.