Abdulrazak Gurnah

Abdulrazak Gurnah Al Kindi (amezaliwa Zanzibar, 20 Desemba 1948[1] ) ni mwandishi mwenye asili ya Zanzibar aliyeishi nchini Uingereza tangu mwaka 1968. Huko anafundisha katika Chuo Kikuu cha Kent tangu mwaka 1982.

Abdulrazak Gurnah

Tangu mwaka wa 1987 alitolea riwaya kadhaa kwa lugha ya Kiingereza. Mwaka 2021 alipewa tuzo ya Nobel ya Fasihi[2][3].

Maisha yake

Abdulrazak Gurnah alizaliwa katika Usultani wa Zanzibar, ambao kwa sasa ni sehemu ya Tanzania.[4] Alifika Uingereza mwaka 1968 baada ya kukimbia Zanzibar kutokana na machafuko yaliyowalenga watu wenye asili ya Kiarabu wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar. [5][6] Gurnah amewahi kusema, 'Nilikuja Uingereza wakati ambao maneno kama "asylum-seeker" hayakuwa yakitumika sana kama wakati huu, watu wengi zaidi wanateseka na kukimbia nchi za kigaidi.'[7] [8]

Alipofika Uingereza alianza kusoma kwenye Chuo cha Christ Church College, Canterbury, baadaye akahamia Chuo Kikuu cha Kent alipopata shahada ya uzamili katika fasihi mnamo 1982. Tasnia yake ilikuwa kuhusu Criteria in the Criticism of West African Fiction.

Kuanzia mwaka 1980 hadi 1983, Gurnah alifundisha kwenye Chuo Kikuu cha Bayero mjini Kano, Nigeria. Akarudi Uingereza akawa profesa wa fasihi hadi alipostaafu [9].

Kazi zake

Hadithi nyingi zilizosimuliwa na Gurnah zinaonyesha mazingira ya pwani ya Afrika ya Mashariki, na wahusika wakuu wa riwaya zake ni wenyeji wa Unguja. Mhakiki wa fasihi Bruce King aliona kwamba Gurnah anaonyesha wahusika wake Waafrika katika uhusiano mpana na Dunia yote, akiwaona kama sehemu za Dunia kubwa inayoendelea kubadilikabadilika. Kufuatana na King, wahusika wa Gurnah mara nyingi ni watu walioondolewa katika asili zao, wanaokataliwa na jamii na kujisikia kama wahanga wa maisha[10]. Mhakiki Felicity Hand aliona kuwa riwaya za Admiring Silence, By the Sea na Desertion, zote zinajadili hisia za kuwa mgeni na kukosa ndugu zinazotokea kwa watu waliopaswa kuondoka kwao na kukaa ugenini. [11]

Tuzo na heshima

Gurnah ndiye mshindi wa tuzo ya Nobel ya fasihi ya mwaka 2021. [12][13] Alichaguliwa kuwa mmoja wa wanajumuiya ya kitaaluma ya fasihi ya Royal Society of Literature mwaka 2006.[14] Mwaka 2007 alishinda tuzo ya RFI Witness of the world nchini Ufaransa kupitia riwaya yake ya By the Sea.[15]

Tuzo nyingine alizowahi kushinda ni pamoja na tuzo ya waandishi wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Writers Prize (Eurasia Region, Best Book)) mwaka 2006, tuzo ya kitabu ya Los Angeles Times kwenye kundi la tamthiliya mwaka 2001 na tuzo ya Booker mwaka 1994.[16]

Orodha ya riwaya zake

Tanbihi

Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Abdulrazak Gurnah kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.